LIBERIA-SIASA-UCHUMI

Rais George Weah amtimua Waziri wake wa Sheria

Rais mpya wa Liberia, George Weah, na Rais anayemaliza muda wake Ellen Johnson Sirleaf wakati wa sherehe za kukabidhiana madaraka Januari 22, 2018.
Rais mpya wa Liberia, George Weah, na Rais anayemaliza muda wake Ellen Johnson Sirleaf wakati wa sherehe za kukabidhiana madaraka Januari 22, 2018. REUTERS/Thierry Gouegnon

Rais mpya wa Liberia George Weah amemfuta kazi Waziri wa sheria Charles Gibson, baada ya malalamishi kuwa amepokonywa leseni ya uwakili baada ya kumtapeli mteja wake.

Matangazo ya kibiashara

Kabla ya uteuzi wake, Gibson alipatikana na hatia hiyo na Mahakama ya Juu baada ya kumtapeli mteja wake Dola za Marekani 25,000 na kuagizwa kuzirejesha.

Rais Weah amemteua Musa Dean aliyekuwa Wakili katika Tume ya Uchaguzi kuchukua nafasi hiyo.

Mwanasoka huyo wa zamani wa Liberia alichaguliwa kuwa rais mteule ikiwa ni katika jaribio lake la pili toka awanie urais wa nchi hiyo.

Weah alichukua nafasi ya Ellen Johnson Sirleaf ambaye alikuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia ambaye alikabidhi madaraka kwa amani.

Rais Sirleaf alimshinda Weah katika uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika mwaka 2005, baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa nchini humo.