CUBA-SIASA

Miguel Diaz-Canel kumrithi Raul Castro

Cuba inajiandaa kufungua ukurasa mpya na kufunga ukurasa wa familia ya Castro kwenye uongozi wa nchi. Baada ya Fidel, kisha Raul Castro, ndugu wawili wameongoza kisiwa hiki chenye utawala wa kikomunisti tangu mapinduzi ya mwaka 1959.

Rais Raul Castro (kushoto) na Makamu wake, Miguel Diaz-Canel baada ya kuwasili katika jengo la Bunge tarehe 18 Aprili 2018, Havana.
Rais Raul Castro (kushoto) na Makamu wake, Miguel Diaz-Canel baada ya kuwasili katika jengo la Bunge tarehe 18 Aprili 2018, Havana. Irene Perez/Courtesy of Cubadebate/Handout via Reuters.
Matangazo ya kibiashara

Miaka sita baadaye, utawala wa kikomunisti bado uko madarakani, lakini Raul anatarajia kuachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa mtu mwengine.

Tangu Jumatano asubuhi, Aprili 18, wabunge wamekusanyika kwa siku kadhaa kwa lengo la kuwachagua viongozi kadhaa kwa nafasi muhimu, ikiwa ni pamoja na kwenye nafasi ya rais. Hata hivyo mrithi wa Raul Castro anatarajiwa kuteuliwa kabla ya Alhamisi wiki hii, lakini mgombea mmoja pekee kwenye nafasi hiyo ni Miguel Diaz-Canel.

Miguel Díaz-Canel, ambaye ni Makamu wa rais wa Cuba, ametajwa na viongozi wa ngazi za juu nchini humo kuwa ndiye kiongozi mtarajiwa ajaye anayekuja kumrithi ama kuchukua nafasi ya Raul Castro.

Miguel anatajwa kuwa na miaka hamsini na mitano, ambaye kwa taaluma ni mhandisi wa zamani anatarajiwa kuchukua ofisi hii leo, baada ya zoezi la upigaji kura rasmi na mkutano wa kitaifa kuidhinisha uteuzi wake.

Raul Castro atasalia kuwa kiongozi mkuu wa Chama cha Kikomunisti mwaka 2021 mpaka mkutano mkuu ujao na anatarajiwa kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii yake.

Miguel Diaz-Canel. ambaye ni mtu wa karibu wa bwana Castro, kwa miaka mitano iliyopita, amekuwa akiandaliwa kushika hatamu za uongozi katika nafasi ya rais.