IRAN-MAREKANI-VIKWAZO-UCHUMI

Rais wa Iran apuuzia mbali vikwazo vya kiuchumi vya Marekani

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema haiwezi kuzungumza na serikali isiyoaminika ya Marekani, wakati huu Washington ikiirejeashea vikwazo vya kiuchumi.

Rais Rohani aahidi kulipiza kisasi dhidi ya vikwazo vya Marekani, Agosti 6, 2018.
Rais Rohani aahidi kulipiza kisasi dhidi ya vikwazo vya Marekani, Agosti 6, 2018. IRANIAN PRESIDENCY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo ya rais Rouhani imekuja, wakati huu Marekani inapoanza kutekeleza vikwazo vya kiuchumi ilivyokuwa imeondoa mwaka 2015 , baada ya uongozi wa zamani wa aliyekuwa rais Barack Obama na mataifa makubwa ya bara Ulaya kutia saini mkataba na Iran kuhusu mradi wake wa nyuklia.

Kiongozi huyo wa Iran amesisitiza kuwa, hawezi kuzungumza na Marekani ambayo ameifananisha na mtu anayemchoma mtu kisu na kukiacha mwilini mwa adui yake.

Uamuzi wa Marekani umekuja baada ya rais Donald Trump kujiondoa kwenye mkataba huo wa kimataifa ambao unalenga kuifanya Iran kutoendelea na mpango wake wa nyuklia kwa muda wa miaka 10.

Trump amekuwa akisema Iran inasalia hatari kwa usalama wa dunia na hivyo nchi hiyo inastahili kutengwa kiuchumi, hatua ambayo imepongezwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye amekuwa akisema nchi yake inaendelea kulengwa na Iran.