DRC-UCHUMI

Tshisekedi aombwa kuingilia kati kuhusu urasibu wa Gecamines

Lori katika mgodi huko Lubumbashi, kusini mashariki mwa DRC (Februari 2014).
Lori katika mgodi huko Lubumbashi, kusini mashariki mwa DRC (Februari 2014). AFP PHOTO / MARC JOURDIER

Wafanyakazi wa kampuni kubwa ya madini nchini DRC Gecamines wamemtaka rais mpya wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi, kuingilia kati uongozi wa kampuni hiyo ambayo wamesema inakabiliwa na "usimamizi wa aibu" tangu ikabidhiwe mkuu wa shirikisho la wafanyabiashara katika jimbo la Katanga, Albert Yuma.

Matangazo ya kibiashara

Wafanyakazi hao wa Gecamine wanasema kampuni hiyo kubwa ya madini ambayo tangu zamani imekuwa ni kitovu cha uchumi wa taifa hilo kubwa na tajiri Afrika, imewanufaisha kwa kiwango kikubwa familia ya rais mstaafu Joseph Kabila na mkuu huyo wa shirikisho la wafanyabiashara, FEK, Albert Yuma ambaye ni mshirika wa karibu wa Kabila.

Kampuni hiyo inayozalisha madini ya Cobalt, shaba na dhahabu kutoka Katanga kusini-mashariki mwa DRC imekuwa chini ya usimamizi wa mfanyabiashara Albert Yuma, tangu mwaka 2010.

Wafanyakazi wa Gecamine wamewasilisha malalamiko yao mbele ya rais Felix Tshisekedi Tshilombo wakimtaka kufanya ukaguzi wa ndani ya kampuni hiyo, ambapo wamemtuhumu kiongozi wao kwa kuhusika na ufisadi, pia ubadhirifu wa mali za serikali pamoja na kuchelewesha mishahara yao.

Hata hivyo hakuna tamko lolote kutoka kwa uongozi wa kampuni hiyo kuhusu tuhuma hizo, wakati wafanyakazi hao wakisubiri uamuzi wa rais Tshisiekedi.