DRC-UBELGIJI-UCHUMI

Tshisekedi awataka wafanyabiasha wa Ubelgiji kuwekeza DRC

Rais wa DRC, Felix Tshisekedi na mkewe Denise wakiwasili Brussels, Ubelgiji kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, Septemba 16, 2019.
Rais wa DRC, Felix Tshisekedi na mkewe Denise wakiwasili Brussels, Ubelgiji kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, Septemba 16, 2019. Benoit DOPPAGNE

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi,amewataka wafanya biashara pamoja na wawekezaji wengine kutoka nchini Ubelgiji kuwekeza nchini mwake kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi hizo mbili.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ambayo ameitoa wakati huu akiendelea na ziara yake ya kikazi nchini humo, ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Ulaya akilenga kurejesha uhusiano kati ya Brussels na Kinshasa.

Serikali ya Ubelgiji ilisitisha uhusiano wake wa karibu na DRC wakati wa utawala wa rais Joseph Kabila waliyekuwa wakimtuhumu kwa kutaka kubadili katiba ili asalie madarakani pamoja na kushindwa kuwakamata watuhumiwa wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ziara ya rais Felix Tshisekedi nchini Ubelgiji ni ishara ya kuanza upya kwa uhusiano baina ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ubelgiji, baada ya kutetereka katika dakika za mwisho za utawala wa rais Joseph Kabila.

Ikulu ya Kinshasa inasema huu ni ukurasa mpya uliofunguliwa, upande wa Ubelgiji wanasema hii ni ziara yenye ishara nzuri ambapo Ubelgiji inafurahishwa na hatua hiyo ya felix Tshisekedi kuzuru kwanza Brussels, Kabla ya Paris katika ziara yake hiyo ya kwanza barani Ulaya, ambapo mwanadiplomasia mmoja wa Ubelgiji amesikika akisema kwamba huu ni udhibitisho wa kudumisha uhusiano wa mataifa hayo mawili.

Hata hivyo baada ya ziara ya mjumbe na maafisa wa Ubelgiji mwezi Mei mwaka huu, hakuna hatua chanya iliopigwa katika uhusiano baina ya pande hizo mbili.