UGANDA-TANZANIA-MAZINGIRA-KILIMO

Tanzania na Uganda wavamiwa na nzige wa jangwani

Nzige wa jangwani wavamia mkoa wa Isiolo, Kaskazini mwa Nairobi nchini Kenya.
Nzige wa jangwani wavamia mkoa wa Isiolo, Kaskazini mwa Nairobi nchini Kenya. RFI/Sébastien Nemeth

Nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kushambuliwa na nzige wa jangwani. Baada ya Somalia na Kenya sasa, Uganda na Tanzania wamevamiwa na nzige hao. Kundi moja la nzige laweza kuharibu chakula cha hadi watu 2,500 kwa siku moja tu.

Matangazo ya kibiashara

Wadudu hao wanaaminika kutokea upande wa nchi ya Kenya ambayo inapakana na nchi hizo mbili.

Maafisa nchini nchini Uganda wamethibitisha uvamizi huo kwa sasa unashuhudiwa katika eneo la Karamoja katika mpaka wa nchi hiyo na Kenya.

Nae Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania Anna Mgwira amethibitisha kuonekana kwa kundi la nzige katika baadhi ya vijiji vya Moshi.

Awali serikali ya Tanzana kupitia Waziri wake wa Kilimo, Japhet Hasunga, iliwahakikishia wakulima na watanzania kwa ujumla kuwa Tanzania haijavamiwa na Nzige wa Jangwani kama inavyoripotiwa na mitandao mbalimbali ya kijamii.

“Hakuna taarifa za kitaalamu zilizothibitisha uwepo wa nzige kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Ila ni kweli Kuna nzige wameonekana Kaunti ya Kajiado nchini Kenya takribani kilomita 50 toka mpakani na Tanzania" alisema Bw Hasunga.

Wadudu hao walidaiwa kupatikana katika eneo la mashariki la wilaya ya Amudat inayopakana na Kenya siku ya Jumapili.

“Uvamizi huu wa nzige ndiyo mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 70, “ Kulingana na shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Mataifa mengine ambayo yameathriwa na nzige ambao wameharibu mimea ni pamoja na Kenya, Somalia na Ethipoia.