Coronavirus: White House na Bunge la Seneti wafikia makubaliano kuhusu mpango wa kuinua uchumi
Imechapishwa:
Baada ya siku kadhaa za mazungumzo, hatimaye Bunge la Seneti la Marekani limefikia makubaliano kati ya pande mbili (Democrats na Republican) kuhusu mpango wa kihistoria wa dola Trilioni 2 kusaidia kukabiliana na janga Covid-19 (Corona) nchini humo.
Mapema wiki hii mpango huo ulikwama bungeni baada ya wabunge kutoka chama cha Republican na wale kutoka chama cha Democratic kushindwa kuelewana.
“Tutapitisha muswaada huo baadaye leo, "Seneta kutoka chama cha Republican, Mitch McConnell, amesema.
Makubaliano baadaye yatatishwa na Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Democratic kabla ya kutiliwa saini na rais wa Marekani, Donald Trump, shirika la habari la AFP limebaini.
Marekani imeandaa mpango kabambe wa kuinua uchumi wake ili kukabiliana na ugonjwa hatari wa Covid-19, ambao shirika la Afya Duniani liliutaja hivi karibuni kuwa ni janga la kimataifa.
Marekani ambayo ni nchi ya kwanza yenye uchumi mkubwa duniani inasema iko tayari kutoa Dola Trilioni 2 ili kusaidia makampuni mbalimbali.