OPEC-UCHUMI

Nchi za OPEC zakubaliana kupunguza kiwango cha uzalishaji mafuta

Mitambo ya mafuta ya Abqaiq, mali ya kampuni ya Aramco nchini Saudi Arabia (picha ya kumbukumbu).
Mitambo ya mafuta ya Abqaiq, mali ya kampuni ya Aramco nchini Saudi Arabia (picha ya kumbukumbu). Fayez Nureldine / AFP

Nchi zinazozalisha mafuta ikiwemo Urusi zimekubaliana kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo kwa asililia kumi  ili kukabiliana na bei ambazo zimeyumba kutokana na athari hasi za Corona.

Matangazo ya kibiashara

Mataifa hayo yamekuwa yakizungumza kwa siku nne zilizopita kabla kuridhia shinikizo la rais wa Marekani Donald Trump  kutaka bei za mafuta kutathminiwa upya.

Kudorora kwa uchumi hali iliyo sababishwa na janga la Covid-19 kumesababisha bei ya mafuta kushuka kwa kiwango cha chini kabisa. Bei ya mafuta imeshuka kwa zaidi ya 50% tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Baada ya siku kadhaa za mazungumzo na mikutano kadhaa ambayo haikuzaa matunda yoyote, hatimaye OPEC, Jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta duniani na washirika wake wamefikia makubaliano Jumapili jioni.

Watapunguza kiwango cha uzalishaji kwa karibu mapipa milioni 10 kwa siku.

OPEC na washirika wake watapunguza kiwango cha uzalishaji wao kwa mapipa milioni 9.7 kwa siku kuanzia mwezi Mei, waziri wa Mexico ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter.

Kauli hii ni muhimu kwa sababu ni sawa na sehemu ambayo Mexico ilikuwa inataka. Hatimaye Mexico imefanikiwa na itapunguza kiwango cha uzalishaji wake kwa mapipa 100,000 tu kwa siku.