UNSC_CORONA-AFYA

Coronavirus: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laendelea kutafuta suluhisho la pamoja

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. REUTERS/Carlo Allegri

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa wiki ijayo kupitisha azimio la kwanza juu ya janga la maambukizi ya Corona, licha ya mivutano kati ya Marekani, China na Urusi.

Matangazo ya kibiashara

Baraza la Usalama limekuwa kimya juu ya janga kubwa kabisa katika historia ya dunia tangu kumalizika vita vikuu vya pili. Baraza hilo limekutana mara moja tangu kulipuka janga la Covid-19. Lilifanya mkutano wake tarehe 9 mwezi huu wa April kutokana na pendekezo la Ujerumani na Estonia.

Azimio lililopendekezwa kwa pamoja na Tunisia na Ufaransa linatoa mwito wa kuimarisha juhudi za pamoja baina ya mataifa yote, pia linatoa mwito wa kukomesha uhasama na mapigano kwenye maeneo ya mizozo.

Lengo la azimio hilo ni kuunga mkono juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanayopambana ili kuzuia maakumbizi ya virusi vya corona na athari zake za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Haijafahamika iwapo azimio hilo litaziwajibisha nchi zote wanachama na kuleta manufaa kwenye sehemu za mizozo kama vile katika baadhi ya nchi za Afrika, Mashariki ya Kati, Afghanistan, Colombia, Syria na Yemen.