Ripoti: Mzunguko haramu wa fedha waifanya dunia kukosa imani kwa taasisi za Afrika
Bara la Afrika limepoteza karibu Dola za Marekani Bilioni 836 kwa kipindi cha miaka 15 hadi kufikia mwaka 2015 katika mzunguko haramu fedha kama vile ukwepaji kodi na wizi kwenda nje ya bara hilo.
Imechapishwa:
Ripoti hiyo yenye kurasa 248, iliyotolewa na Tume ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD inaeleza kuwa, mzunguko huo haramu wa fedha unahusishwa na usafirishaji wa madini kama Almasi, Dhahabu pamoja na visa vya ufisadi na watu kukwepa kulipa kodi.
Aidha, ripoti hiyo inaeleza kuwa, bara la Afrika linapoteza karibu Dola billioni 89 kila mwaka kutokana na mzunguko huo.
Pamoja na hayo, Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa, inaeleza kuwa fedha zinazopotea ni zaidi ya zile ambazo bara la Afrika inapata kutoka kwa wahisani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katibu Mkuu wa UNCTAD, Mukhisa Kituyi amesema kuwa mzunguko huo haramu wa fedha kutoka barani Afrika, unawaibia Waafrika na kuifanya dunia kukosa imani kwa taasisi za Afrika, huku Waafrika wengi wakiendelea kuwa maskini na kushindwa kupata mahitaji muhimu kama afya bora na elimu.