Wizara ya Michezo nchini Ufaransa yamsafisha Kocha wa Timu ya Taifa Laurent Blanc na tuhuma za ubaguzi wa rangi
Imechapishwa:
Wizara ya Michezo nchini Ufaransa imemsafisha Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Laurent Blanc na tuhuma za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zinazomzingira baada ya kunukuliwa wakati akichagua wachezaji wa timu ya taifa.
Waziri wa Michezo wa Ufaransa Chantal Jouanno ndiye ambaye amechukua jukumu hilo la kumsafisha Blanc ambaye alikuwa kwenye wakati mgumu wa kutakiwa kujibu ni kwa nini ametumia maneno ya kibaguzi dhidi ya wachezaji wenye asili ya Afrika.
Jouanno amemuambia mkutano wa wanahabari kuwa hakuna ushahidi wa kutosha ambao unawapa nguvu za kuweza kutoa adhabu ya ubaguzi wa rangi kwa Blanc.
Tamko hili la kumsafisha Blanc linakuja siku moja baada ya jumatatu Blanc kusikilizwa na Shirikisho la Soka Nchini Ufaransa FFF pamoja na Waziri wa Michezo juu ya tuhuma ambazo zinamkabili na yeye kutakiwa kujitetea.
Jouanno bila ya kupoteza muda aliwaambia wanahabari ambao walijitokeza kusikiliza hukumu ambayo ingetolewa baada ya kusikilizwa shauri hilo na yeye akawaambia hakuna umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Blanc.
Waziri huyo wa Michezo akaenda mbali zaidi na kusema hakuna ushahidi ambao unaonesha Kocha huyo wa Timu ya Taifa amevunja sheria ya Ubaguzi wa rangi ya mwaka 2001.
Jouanno hakusita kumwagia sifa Blanc ambaye alichukua nafasi kutoka kwa mtangulizi wake Raymond Domenech na kusema ameweza kurejesha heshima ya timu hiyo ambayo ilianza kushuka.
Wachezaji ambao walimuunga mkono Blanc kwa kile ambacho alikifanya ni pamoja na Zinedine Zidane, Christophe Dugarry, Marcel Desailly, Bixente Lizarazu na Kocha ambaye aliwasaidia Ufaransa kushinda Kombe la Dunia mwaka 1998 Aime Jacquet.
Wakati wachezaji hao ambao walikuwepo kwenye kikosi cha mwaka 1998 alichocheza pia Blanc lakini Lilian Thuram na Patrick Vieira pekee ndiyo ambao walimkoa vikali Kocha huyo wa sasa kutoka na kutoa maneno yake ambayo yanatuhumiwa kuwa ni ya kigabuzi.