MAREKANI

Kukamatwa kwa Strauss-Kahn Kutoathiri kikao cha mawaziri wa umoja wa ulaya

(Photo : Reuters)

Sakata la kukamatwa kwa mkuu wa shirika la fedha duniani Dominique Strauss-Kahn limeghubika kikao cha mawaziri wa fedha wa umoja wa ulaya ambao wanatazamiwa kuketi baadae leo kupitisha mkopo kwa Ureno , kuzungumzia mzigo wa madeni unaoendelea kuiandama Ugiriki na kuchagua rais mpya wa benki ya umoja huo.

Matangazo ya kibiashara

Bwana Kahn ambaye amekuwa akiongoza juhudi za kimataifa kunusuru uchumi wa bara la ulaya ili usiathiri uchumi wa dunia  alikuwa aongoze kikao  hicho  kinachotazamiwa kuanza  saa saba kamili mchana kwa saa za kimataifa.

Taarifa kutoka IMF zinaeleza kuwa kaimu wa bwana Kahn, Nemat Shafik sasa ataongoza kikao hicho cha mawaziri hao kitakachodumu kwa siku mbili.

Wachambuzi wa mambo wanasema kukamatwa kwa bwana Kahn kunaweza kusiathiri  mchakato wa mkopo wa Ureno na kwamba waliopata pigo kubwa katika sakata hilo ni ugiriki ambao wana mahusiano mazuri na kiongozi huyo.

Tetesi zimeibuka katika siku za hivi karibuni kuwa Ugiriki itahitaji mkopo mwingine wa dola bilioni themanini na tano   katika kipindi cha miaka miwili ijayo kwa kuwa bado haijawa tayari kurejesha mkopo wa euro bilioni mia moja na kumi iliyokopa mwaka jana.

Wakili wa bwana Kahn, William Taylor amesema mteja wake amekubali kufanyiwa uchunguzi wa  kitaalam kubaini endapo alijaribu kumbaka mhudumu wa hoteli.

Sakata hilo linazidi kupata sura mpya kila kukicha na sasa  mwandishi wa vitabu  Tristane Banon naye anajipanga kumfungulia mashtaka bwana Khan kwa madai ya kumdhalilisha mwaka 2002.

Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo wa IMF kutuhumiwa kwa makosa hayo ya kudhalilisha wanawake na wakati huu tuhuma hizo zinaonekana kuzima ndoto ya bwana Kahn kuwania urais wa Ufaransa.

Wanasiasa wa ufaransa  wakiwemo wanasiasa kutoka  chama tawala  UMP wameanza kutilia shaka taswira ya Ufaransa katika dunia kutokana na tukio hilo.