Italia

Waziri mkuu wa Italia apata pigo kubwa

Silvio Berlusconi akubali kushindwa kura ya maoni
Silvio Berlusconi akubali kushindwa kura ya maoni REUTERS/Stefano Rellandini

Kushindwa kwa Waziri mkuu Silvio Berlusconi, katika kura za maoni nchini Italia, kumepokewa kwa maswali mengi na washirika wa kiongozi huyo anayekabiliwa na kashfa za aina mbalimbali.

Matangazo ya kibiashara

Gazeti la Il Giornale, linalomilikiwa na familia ya Berlusconi linasema pasina kificho, kuwa hizi ni nyakati ngumu kwa serikali ya muungano ambayo, imejikuta dhoofu, kufuatia matokeo ya kura hizo.

Kwa mara ya kwanza kabisa, Berlusconi, kiongozi aliyekuwa na nguvu nchini Italia kwa takriban miaka 20, sasa anaonekana kupingwa na wapiga kura wake.

Kufuatia zoezi la kura za maoni, lililofanyika siku ya Jumapili na Jumatatu, asilimia 94 ya wananchi wanaona si jambo jema taifa hilo kuzalisha nguvu za nyuklia, wala kutoa kinga ya kushtakiwa mahakamani kwa viongozi wa serikali.

Na wakati wanaomkosoa Berlusconi wakiandamana huku na huko wakisherehekea mabadiliko katika siasa za Italia, waziri mmoja kutoka Chama cha League Roberto Calderoli, amesema walilopata ni kofi kali shavuni, pigo ambalo walilipata pia katika uchaguzi majuma mawili yaliyopita.