Maandamano zaidi yaendelea nchini Hispania
Imechapishwa:
Maandamano zaidi yameendelea nchini Hispani katika miji mbalimbali nchini humo, maandamano yanayolenga kupinga hali mbaya ya kiuchumi nchini humo na ukosefu wa ajira.
Maandamano hayo ambayo yalianza siku ya Jumamosi kwa wananchi kutembea kwa miguu toka miji mbalimbali nchini humo wakielekea katika mji wa Madrid ambako wameweka kambi kuishinikiza serikali yao kutatua tatizo la ajira kwa vijana nchini humo.
Siku ya Jumapili mji wa Madrid ulifurika maelfu ya waandamanaji ambao wengine waliwasili wakiwa katika mabasi wakiimba nyimbo za kukejeli serikali huku wengine wakishika mabango yenye ujumbe wa kumtaka waziri mkuu wa nchi hiyo kusikia kilio cha wananchi.
Viongozi wa maandamano hayo wamesema kuwa wanapinga kitendo cha wanasiasa nchini humo kushindwa kutekeleza sera ambazo walitangaza wakati wa uchaguzi mkuu nchini humo wakitaka viongozi hao kujiuzulu.
Tayari wanaharakati nchini humo wametangaza kuunga mkono maandamano hayo na kuahidi kuendelea kuyaunga mkono kwa lengo la kukosoa sera za serikali.