Waziri mkuu wa zamani wa Ukrain ahukumiwa kifungo cha miaka saba jela
Waziri mkuu wa zamani wa Ukrain Yulia Tymoshenko amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka kipindi alipokuwa madarakani ikiwemo kusaini mkataba wa nishati ya gesi na nchi ya Urussi mwaka 2009
Imechapishwa:
Akitoa hukumu hiyo jaji Rodion Kireyev amesema kuwa pamoja na kwenda jela miaka saba Tymoshenko atarejesha dola milioni 186 ambazo taifa hilo lilipoteza kufuatia kusaini mkataba wa nishati ya gesi huku akifungiwa kushiriki katika masuala ya kisiasa kwa miaka mitatu
Kwa upande wake waziri huyo wa zamani,amesema kuwa tuhuma dhidi yake ziliendeshwa kisiasa na ameapa kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa ambapo atapeleka kesi hiyo katika mahakama ya haki za binadamu nchini Ulaya
Aidha Tymoshenko ameahidi kuipigania nchi ya Ukraine hadi mwisho wa maisha yake na kurejesha heshima ya jina lake
Nchi ya Marekani na umoja wa Ulaya zimelaani hukumu hiyo na kusema kuwa tuhuma dhidi ya mwanamke huyo zilikuwa za kibaguzi na za kisiasa na kwamba kufungwa kwa Tymoshenko kutaondoa kabisa matumaini ya kujenga uhusiano baina ya nchi hiyo na umoja wa Ulaya
Polisi wa kuzuia ghasia walisimama nje ya mahakama wakati maelfu ya wanaomuunga mkono mwanamke huyo pamoja na wapinzani wake walipofika kushuhudia kesi hiyo ambapo imeripotiwa kuwepo kwa vurugu chache na watu wachache kukamatwa