Ufaransa

Mfaransa aliyetekwa nchini Kenya Marie Dedieu amefariki nchini Somalia

REUTERS/Handout/Files

Mwanamke wa Ufaransa Marie Dedieu aliyetekwa nchini Kenya na wanaosadikiwa kuwa ni wanamgambo wa Somalia mapema mwezi huu amefariki dunia wamesema maafisa wa Serikali ya Ufaransa. Wanadiplomasia wa Ufaransa wamesema kuwa walipata taarifa za kifo cha mwanamke huyo kupitia kwa watu waliokuwa wakiwasiliana nao kwa ajili ya kuweka makubaliano ya kuachiwa kwa Marie Dedieu.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo tarehe kamili ya kifo cha mwanamke huyo haijajilikana na inahisiwa kuwa kudhoofika kwa afya yake kulikosababishwa na kukosekana kwa matibabu huenda ikawa ndiyo chanzo cha kifo chake.

Marie Dedieu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 66 alikuwa miongoni mwa raia wa nchi za magharibi walitekwa wakiwa mjini Lamu nchini Kenya mapema mwezi huu wa Oktoba.

Matukioa ya kutekwa kwa watalii yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini Kenya na hata kutishia sekta ya utalii kutokana na kuwepo kwa hali ya wasiwasi kuhusu usalama.

Kufuatia vitendo hivyo Serikali ya Kenya imeamua kuwasaka wanamgambo wa kundi la Al -Shabab ambao wadaiwa kuwa wanafanya vitendo hivyo vya utekaji wa watalii.