UGIRIKI-ATHENS

Serikali ya waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou hatarini kuvunjika

Waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou akizungumza na waandishi wa habari alipohudhuria mkutano wa G20
Waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou akizungumza na waandishi wa habari alipohudhuria mkutano wa G20 Reuters

Hali ya mambo imeendelea kumwendea kombo waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou ambapo sasa huenda akalazimika kuivunja serikali yake kutokana na mpango wake wakuitisha kura ya maoni kutoungwa mkono na wabunge wengi.

Matangazo ya kibiashara

Katika kile kinachoonekana ni kufikia ukingoni kwa siasa za Papandreou, kiongozi huyo ameendelea kupata upinzani mkali toka kwa wabunge na mawaziri wanaounda serikali yake ambapo sasa kumetokea mgawanyiko mkubwa kati yao na huenda akalazimika kuivunja serikali yake.

Kuitishwa kwa kura ya maoni nchini Ugiriki kulitokana na shinikizo toka kwa wananchi ambao wanataka kupigwa kura kuamua endapo nchi hiyo iendelee kuwepo kwenye Umoja wa Ulaya au la, hatua iliyowakasirisha viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wanaotaka nchi hiyo kuamua sasa.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa huenda huu ukawa mwisho wa Papandreou kuiongoza nchi hiyo kwakuwa anamiliki uungwaji mkono wa karibu viti 152 kati ya 300 kitu ambacho wanaona kuwa huenda ndicho kitaiangusha serikali hiyo.

Imeelezwa kuwa muda mchache ujao waziri mkuu huyo anatarajiwa kukutana na rais wa nchi hiyo na inaelezwa kuwa anafanya hivyo kwa lengo la kutaka kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwake na hatomaye kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.