UGIRIKI

Waziri mkuu mpya wa Ugiriki aahidi kutafuta ushirikiano.

Waziri mkuu mpya wa Ugiriki Lukas Papademos
Waziri mkuu mpya wa Ugiriki Lukas Papademos REUTERS/Yiorgos Karahalis

Baraza la mawaziri linaloongozwa na waziri mkuu mpya wa Ugiriki Lucas Papademos linatarajiwa kula kiapo ijumaa hili huku akiahidi kuunda ushirikiano ili Ugiriki iendelee kubaki ndani ya umoja wa ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Waziri huyo ambae aliwahi kuwa makamu wa rais wa zamani wa benki ya ulaya, EU mwenye umri wa miaka 64 aliteuliwa jana baada ya wanasiasa nchini humo kuafikiana uteuzi wake na kutakiwa kuunda serikali ya mpito ya muungano

Rais wa Ugiriki Karolos Papoulias alimteuwa waziri mkuu huyo mpya baada ya mapendekezo ya viongozi wa kisiasa ambao walihudhuria mkutano wa jana.

Akiongea kwa mara ya kwanza baada ya uteuzi wake Papademos amesema nchi ya Ugiriki ipo katika njia panda, na ameahidi kuendelea kuwa katika Umoja wa Ulaya.

Papademos ataiongoza serikali ya mpito ya nchi hiyo mpaka pale uchaguzi utakapofanyika mwezi Februari mwakani, huku kukiwa na taarifa kuwa bado hakujawa na makubaliano ya uundwaji wa serikali ya umoja.

Papademos amechukua nafasi ya aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, George Papandreau aliyelazimika kuachia ngazi, baada ya kuitisha kura ya maoni juu ya mpango wa kupata mkopo wa fedha ili kulinusuru taifa hilo na mzigo wa madeni.