ITALIA

Thamani ya Euro yapanda baada ya kuteuliwa kwa Waziri Mkuu mpya wa Italia

REUTERS/Francois Lenoir/Files

Thamani ya sarafu ya Euro, imeimarika dhidi ya sarafu ya Dola ya kimarekani katika masoko ya hisa barani Asia, baada ya aliyekuwa kamishina wa umoja wa Ulaya, EU Mario Monti kupendekezwa kuwa waziri Mkuu mpya wa Italia

Matangazo ya kibiashara

Monti alipendekezwa kuchukua nafasi hiyo ya uwaziri mkuu baada ya kujiuzulu kwa waziri Mkuu wa zamnai Silvio Berlusconi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi nchini humo.

Mario Monti alipendekezwa kuwa wazir Mkuu mpya jana jumapili na rais wa Italia Giorgio Napolitano baada ya kujiuzulu kwa Silvio Berlusconi kutokana na hali hiyo.

Kamishina huyo wa zamani wa umoja wa Ulaya, anatarajiwa kuanza mazungumzo ya kuunda serikali mpya kwa kuliteua baraza la mawaziri.

Monti amewaambia wananchi wa Italia kuwa, analenga kuimarisha uchumi wa taifa hilo ili Italia ipate heshima, kama mwanzilishi wa umoja wa Ulaya.

Kamishina huyo wa zamani amepata uungwaji mkono na idadi kubwa ya wanasiasa nchini humo, kikiwemo chama cha Silvio Berlusconi.

Bunge nchini Italia baadaye juma hili linatazamiwa kupitisha jina na Monti kuwa Waziri Mkuu mpya, huku wananchi nchini Italia wakiwa na matumaini makubwa uzoefu alionao katika maswala ya fedha na uongozi katika Umoja wa Ulaya utasaidia kuinua uchumi wa Italia.