ITALIA

Waziri Mkuu wa Italia kuweka hadharani serikali yake

REUTERS/Tony Gentile

Waziri mkuu mteule wa Italia,Mario Monti amesema kuwa ana uhakika kuwa Italia itaondokana na mzigo wa madeni na kwamba ataiweka wazi serikali yake mpya muda mchache ujao.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani, wafanyabiashara na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, Monti amesema ana uhakika juu ya uwezo wa nchi yake kukabili wakati huu mgumu walionao hivi sasa.

Monti ametoa wito wa kushiriki katika kuhakikisha kuwa uchumi unakua, kuimarika na kudumu kwa muda mrefu huku viongozi wa vyama vya wafanyakazi wakitoa ahadi ya kushiriki kwa kujitoa kwa ajili ya mafanikio hayo.

Mchumi huyo anatarajiwa kukutana na rais wa Italia,Giorgio Napolitano hii leo na kukubali rasmi uteuzi wa kushika wadhifa wa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Silvio Berlusconi,tukio litakalofuatiwa na sherehe za kuapishwa kwake.

Nchi ya Italia inakabiliwa na hali ya kuyumba kwa uchumi kama ilivyo kwa nchi nyingine za Ulaya hali ambayo imesababisha nchi hizo kuanzisha harakati za kuimarisha uchumi na kulinda nguvu ya sarafu ya euro isiporomoke.