HISPANIA

Chama cha upinzani nchini Hispania chashinda uchaguzi mkuu

Kiongozi wa chama cha PP, Mariano Rajoy
Kiongozi wa chama cha PP, Mariano Rajoy Reuters

Chama Kikuu Cha Upinzani nchini Hispania Cha PP kinachoongozwa na Mariano Rajoy kimefanikiwa kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa wabunge uliofanyika hapo jana katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na ukosefu wa ajira.

Matangazo ya kibiashara

Chama Cha Kisoshalisti ambacho kilikuwa kinaongoza nchi hiyo tangu mwaka elfu mbili na nne kimekiri kushindwa kwenye kinyang'anyiro hicho na kutoa nafasi kwa Rajoy kuwa Waziri Mkuu mpya wa taifa hilo.

Rajoy amewaambia wananchi anafahamu fika matatizo wanayokabiliana nayo yakiwemo ukosefu wa ajira na tishio la kuanguka kwa uchumi wa nchi hiyo lakini atafanya kila linalowezekana kukabiliana na hali hiyo.

Chama hicho kimechukua uongozi wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliwa na deni na mtikisiko wa kiuchumu suala ambalo hata wachambuzi wa mambo wameitabiria magumu serikali mpya itakayoundwa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa wananchi wa Hispania wameamua kufanya mabadiliko katika serikali kufuatia kutokuwa na imani na serikali yao ambayo wamekuwa wakiituhumu kwa kushindwa kubadili uchumi wa nchi hiyo na kutengeneza ajira mpya kwa muda mrefu.