IRAN-MAREKANI

Marekani na Uingereza zatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akitangaza uamuzi wa nchi yake kuiwekea vikwazo vipya Iran
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akitangaza uamuzi wa nchi yake kuiwekea vikwazo vipya Iran Reuters/Hyungwon Kang

Mataifa ya Magharibi yakiwemo Marekani, Canada na Uingereza yametangaza vikwazo vipya vya kiuchumi vilivyoilenga nchi ya Iran na kugusa Benki Kuu ya Nchi hiyo pamoja na sekta yake muhimu ya nishati.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo wa mataifa hayo kuweka vikwazo dhidi ya Iran unaopingwa vikali na China na Urusi umekuja baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa UN kuituhumu nchi hiyo kuwa na mpango wa kutengeneza silaha za maangamizi.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amesema kuwa rais Barack Obama kwa mara ya kwanza ametia saini sheria kali ya kuiwekea vikwazo nchi ya Iran ambayo imeendelea kukaidi maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kuitaka nchi hiyo kuachana na mpango wa kurutubisha madini ya Uranium.

Mara baada ya kutangazwa kwa vikwazo hivyo vipya dhidi ya Iran, nchi ya Urusi imesema kuwa haiungi mkono hatua hiyo ya Marekani na washirika wake kwakuwa inakwenda kinyume na maazimio ambayo yalipitishwa na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tangu awali nchi ya Urusi na China zimekuwa mstari wa mbele kuikingia kifua nchi ya Iran na kusababisha maazimio kadhaa ya Umoja huo kushindwa kupitishwa kwasababu ya kura ya veto.