UGIRIKI

Ugiriki yazilalamikia baadhi ya nchi za Ulaya kuhusu mkopo

Serikali ya Ugiriki imezilalamikia baadhi ya nchi za Ulaya na kusema kuwa nchi hizo hazitaki kuwepo kwa Ugiriki ndani umoja wa Ulaya na haziitakii mema nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Evangelos Venizelos amezituhumu nchi hizo na kuongeza kuwa zinachezea moto wakati Ugiriki ikijitahidi kukamilisha masharti iliyopewa na Umoja wa Ulaya, EU pamoja na Shirika Fedha Duniani, IMF ili iweze kupata mkopo.

Hatua hiyo imekuja baada ya nchi za Ulaya kusitisha mpango wake wa kuipa mkopo Ugiriki kwa madai ya kutoridhishwa na jitihada zinazofanywa na nchi hiyo katikam kushughulikia madeni na kubana matumizi.

Awali Tume ya Umoja wa Ulaya iliunga mkono uamuzi wa Bunge la nchi ya Ugiriki kuidhinisha mpango mpya wa hatua zitakazochukuliwa na nchi hiyo katika harakati za kubana matumizi.

Mpango huo umekuja ikiwa ni njia moja wapo ya kukabiliana na madeni na hali mbaya ya kuyumba kwa uchumi nchini humo na katika nchi nyingine za Ulaya.

Kamishina wa Uchumi wa Tume ya Umoja wa Ulaya Olli Rehn amewaagiza maafisa wa Serikali ya Ugiriki kutekeleza mabadiliko hayo yanayotakiwa na umoja wa Ulaya ili Ugiriki ipatiwe mkopo zaidi.

Hatua hizo zilitarajiwa zitaisaidia Ugiriki kufufua uchumi wake kama zitatekelezwa kikamilifu na endapo Ugiriki haitafanya hivyo hali itakuwa mbaya zaidi.