UGIRIKI-UBELGIJI

Benki Kuu ya Ulaya yatoa mkopo wa euro bilioni 530 kusaidia uchumi wa nchi za Ulaya

Nembo ambayo inatumiwa na Umoja wa Ulaya EU iliyopo Makao Makuu huko Brissels nchini Ubelgiji
Nembo ambayo inatumiwa na Umoja wa Ulaya EU iliyopo Makao Makuu huko Brissels nchini Ubelgiji

Benki Kuu Barani Ulaya ECB imetoa euro bilioni mia tano na thelathini kwa ajili ya kusaidia Mabenki mia nane barani humo ili ziweze kuwa na uwezo wa kutoa mikopo na kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi.

Matangazo ya kibiashara

Mkopo huo ni wapili kutolewa na Benki Kuu ya Ulaya ambapo mwezi Desemba mwaka jana jumla ya euro bilioni mia nne na themanini na tisa zilitolewa kuzisaidia Benki hizo kushughulikia tatizo la uchumi na madeni.

Lengo la kutolewa kwa mkopo huu wa euro bilioni mia tano ni kuhakikisha mataifa ya Ulaya ambayo yanapitia kipindi cha kutetereka kwa uchumi yanapata ahueni kwa kuongezewa nguvu kukabiliana na madeni.

Mkopo huu unatolewa wakati huu ambapo mgomo na maandamano yakiendelea kushuhudiwa nchini Ugiriki katika Jiji la Athens ambapo Muungano wa Vyama Vya Wafanyakazi vinapinga masharti ya Umoja wa Ulaya EU.

Benki Kuu ya Ulaya ECB imesema mkopo huo unatolewa lakini nchi ambazo zitachukua fedha hizo ni lazima zihakikishe zinabana matumizi ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi inayoshuhudiwa kwenye mataifa mengi.

Wafanyakazi nchini Ugiriki wamesema hawapo tayari kuona wanaendelea kukabiliwa na hali ngumu huku ajira zao zikiwa mashakani kutokana na serikali kutekeleza masharti ya Umoja wa Ulaya EU ili wapate mkopo huo.

Umoja wa Ulaya EU na Shirika la Fedha la Kimataifa Duniani IMF kwa pamoja wameendelea kushinikiza Ugiriki ni lazima ubane matumizi ili ipate mkopo zaidi na hivyo ndiyo nchi hiyo itaweza kukabiliana na hali waliyonayo kwa sasa.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Lucas Papademos anatarajiwa kukutana na Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya EU Jose Manuel Barroso ili kuweza kujadilinafasi ya nchi hiyo kuweza kupata mkopo zaidi.