Ufaransa

Rais Mteule wa Ufaransa Francois Hollande kuapishwa hii leo

Rais mteule wa Ufaransa Francois Hollande
Rais mteule wa Ufaransa Francois Hollande REUTERS/Charles Platiau

Rais Mteule wa Ufaransa kupitia Chama cha Kisoshalisti Francois Hollande anatarajiwa kuapishwa hii leo kushika wadhifa wa Urais kwa miaka mitano ijayo kabla ya kutaja Waziri Mkuu wa serikali yake na baadae ataelekea nchini Ujerumani kukutana na kansela Angela Marekl kujadili mgogoro wa kiuchumi unaoendelea barani Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Siku tisa baada ya Hollande kumuangusha Rais anayemaliza muda wake wa miaka mitano kwenye duru la pili la uchaguzi wa Urais Nicolas Sarkozy anayetoka mrengo wa kulia kwenye kampeni kali hatimaye anatarajia kuanza rasmi jukumu la kuiongoza Ufaransa.

Hollande anachukua utawala kisha kufunga safari kuelekea nchini Ujerumani kukutana na Kansela Angel Merkel kujadili kwa kina namna ambavyo serikali hizo mbili zinaweza kusaidia kutatua mgogoro wa kiuchumi katika nchi za Ulaya.

Hiyo itakuwa ziara ya kwanza kwa Rais Hollande akiwa Kiongozi wa nchi hiyo huku akiwa na kibarua cha kuhakikisha anaimarisha uchumi wa Taifa hilo kama ambavyo aliwaahidi wananchi wakati wa kampeni zake.

Hollande pia anatarajiwa kumtaja Waziri Mkuu wa serikali yake huku nafasi kubwa akipewa Kiongozi wa Chama Cha Kisoshalisti Jean-Marc Ayrault ambaye anatakuwa na jukumu la kuongoza serikali mpya.