Ugiriki

Chama cha mrengo wa Kushoto nchini Ugiriki,Syriza chasisitiza kutounga mkono Sera ya kubana matumizi

Kiongozi wa Chama cha Syriza, Alexis Tsipras
Kiongozi wa Chama cha Syriza, Alexis Tsipras REUTERS/Kostas Tsironis/Pool

Chama Cha Mrengo wa Kushoto nchini Ugiriki cha Syriza ambacho kilishika nafasi ya pili kwa wingi wa wabunge kwenye uchaguzi uliofanyika nchini humo kimesema msimamo wao juu ya sera ya kubana matumizi utaendelea kusalia pale pale licha ya kukabiliwa na ukosoaji.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa Chama hicho Alexis Tsipras amesema kuwa hawakubaliani na mbinyo ambao wanakutana nao kutoka kwa Umoja wa Ulaya EU pamoja na shinikizo la Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanaowataka wabadili msimamo wao.

Kiongozi huyo wa Chama Cha Syriza amesema sera ya kubana matumizi wanapingana nayo kwa kuwa inasababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi kitu ambacho hawawezi kukiunga mkono ndiyo maana walijitoa kwenye juhudi za kupata serikali ya muungano.

Ugiriki imeshuhudia ikishindwa kufikia muafaka wa kuunda serikali ya muungano na hivyo serikali ya mpito imechaguliwa na itaongozwa na Waziri Mkuu Panagiotis Pikramenos ambayo atalazimika kuongoza hadi uchaguzi utakapofanyika tarehe kumi na saba mwezi Juni.

Hatua ya kuchagua serikali ya mpito imekuja baada ya mazungumzo ya siku tisa kushindwa kufua dafu kufikia muafaka wa kuunda serikali ya muungano baada ya kufanyika uchaguzi wa wabunge na hakuna chama kilichopata wabunge wa kuweza kuwapa fursa ya kuunda serikali peke yao.