ULAYA

Fainali za soka kombe la mataifa ya Ulaya kutimua vumbi Jumapili, Italia yaishangaza Ujerumani

RFI

Fainali za Euro 2012, zinatazamiwa kufikia mwisho siku ya Jumapili hii, yaani Julai Mosi, ambapo Italia itachuana na Uhispania na huu utakuwa ni mtanange ambao unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi katika kila kona ya dunia.

Matangazo ya kibiashara

Italia ilifikia hatua hiyo ya fainali baada ya kupata ushindi wa bao 2-1 timu ya Ujerumani katika mchezo wa nusu fainali ambao ulikua wa vuta nikuvute huku kila timu ikiwania ushindi katika mechi hiyo iliyokuwa muhimu kwa kila timu.

Mario Balotelli alifunga magoli mawili na kuiwezesha timu yake ya Italia kuishangaza Ujerumani kwa ushindi huo wa magoli 2-1 katika nusu fainali ya Euro 2012 na hivyo kupata nafasi ya kucheza mechi ya fainali mjini Kiev dhidi ya Uhispania.

Timu hiyo ya meneja Cesare Prandelli ilistahili ushindi, kwani sio tu waliweza kupambana na Ujerumani ambayo iliwashinda wapinzani wao kwa urahisi, bali pia walifunga mabao yao mapema katika kipindi cha kwanza.

Balotteli amekuwa ni mchezaji wa kwanza kutoka barani Afrika kujipatia sifa katika soka huko Italia na kuwavuta mashabiki wengi hasa zaidi kwa namna ambavyo anavyonyoa nywele zake.

Balotteli amesema kuwa kilichomvutiya zaidi ilikuwa ni kumwona mama yake uwanjani,halafu kaongeza kuwa atajitahidi kuhakikisha anafanya vizuri zaidi endapo atamwona babake anakuja kushuhudia fainali hapo siku ya Jumapili.

Mashabiki wa soka wanasema kuwa Italia kamwe hawajawahi kushindwa na Ujerumani katika mashindano makubwa, na wamefanikiwa sasa kucheza mechi nane dhidi ya Ujerumani pasipo kushindwa.