INDIA-PARIS

Ufaransa na India zaafikiana kuhusu ununuzi wa ndege za kivita

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh wameafikiana kuhusu mradi wa ununuzi wa ndege za kivita zenye thamani ya Dola Bilioni 12.

Matangazo ya kibiashara

Hollande na Singh wamesema kuwa mazungumzo yao yamezaa matunda na sasa India itakuwa katika nafasi nzuri ya kununua ndege hizo kutoka Ufaransa.

Serikali ya Paris na ile ya  New Delhi zimekuwa zikijadiliana kuhusu biashara hiyo kwa kipindi kirefu inayoelezwa na serikali hizo mbili kuwa yenye thamani kubwa zaidi duniani kijeshi.

Rais Hollande amezuru India  katika ziara yake ya kwanza barani Asia na nchini humo tangu alipochaguliwa kuwa rais mwaka uliopita na mbali na maswala ya ununuzi wa ndege za kivita, viongozi hao pia wamejadili maswala ya Nyuklia baina ya mataifa hayo mawili.

Mwaka uliopita,  India iliichagua kampuni moja ya kutengeza ndege za kivita kutoka Ufaransa ili kuimarisha usalama wa angaa lake.

Wahandisi kutoka Ufaransa pia wamepewa mkataba wa kujenga kituo kikubwa cha Nyuklia chenye Megawatt zaidi ya elfu tisa za kuzalisha  Magharibi mwa nchi hiyo makubaliano yaliyotiwa saini kati ya mataifa hayo mawili mwaka 2010.

Mbali na hayo, Rais Hollande amemwambia Waziri Mkuu Singh kuwa Ufaransa inaunga mkono juhudi za India kujumuishwa katika Baraza la Usalama la Umoaj wa Mataifa.