JAPAN

Japan yaadhimisha miaka miwili tangu kutokea kwa Tsunami

Wananchi wa Japani jumatatu hii wanaadhimisha miaka miwili tangu kutokea kwa janga la Tsunami, maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na kumbukumbu ya vifo vya watu takribani elfu 19 ambao waliangamia katika tukio hilo la kihistoria.

Reuters
Matangazo ya kibiashara

Utulivu umetawala katika shule ya Ishinomaki eneo ambalo wanafunzi wapatao 70 walikumbwa na umauti baada ya kusombwa na maji mwezi machi mwaka 2011.

Maadhimisho hayo yanafanyika katika miji mbalimbali nchini humo wakati Waziri Mkuu Shinzo Abe akiahidi kutekeleza mipango maalumu itakayowasaidia waathirika na Tsunami.

Serikali imesema kinu hicho kwa sasa kiko imara na hakutaweza kutokea hatari kama iliyojitokeza miaka miwili iliyopita, na imethibitisha kuwa bidhaa za chakula zinafanyiwa uchunguzi kwanza kubaini kama kuna mionzi kabla ya kuingizwa sokoni na kuwafikia walaji.

Licha ya hakikisho hilo bado kumekuwa na hofu, wateja wengi wanajiepusha kutumia bidhaa za Fukushima kutokana na kuhofia usalama wa afya zao.

Jitihada za kujijenga upya baada ya Tsunami bado zinasuasua wakati takwimu zikionyesha kuwa watu 315,196 hawana makazi ya kudumu mpaka hivi sasa tangu kutokea kwa janga hilo.

Mwezi March mwaka 2011 nchi hiyo ilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lililosababisha maafa makubwa nchini humo na kupelekea hata kupasuka kwa vinu vyake vya nyuklia vya Fukushima.