UTURUKI

Waasi wa PKK wawaachia huru mateka nane waliokuwa wakiwashikilia kwa miaka miwili

Waasi wa jamii ya Kikurdi, Kurdistan Workers Party (PKK) wamewaachia huru mateka nane wa Uturuki ikiwa ni mwitikio wa mpango mpya wa amani wa Ankara unaolenga kumaliza mgogoro wa miaka 29 katika eneo la kusini mashariki mwa nchi ya Uturuki.

AFP / Files / Joseph Barrak
Matangazo ya kibiashara

Kuachiliwa kwa mateka hao waliokuwa wakishikiliwa kwa miaka miwili kaskazini mwa Iraq kunakuja baada ya kiongozi wa PKK aliye kifungoni Abdullah Ocalan kusema ana matumaini ya kuona wafungwa wanakuwa na familia zao.

Taarifa toka nchini humo zinasema kuwa Ocalan alianza mazungumzo ya siri na Serikali ya Uturuki ili kumaliza mzozo uliodumu kwa miaka 29.

Kiongozi wa ulinzi wa PKK Bawer Pirson, amewaambia waandishi wa habari kuwa wameitikia wito wa kiongozi wao na kuamua kuwaachia wafungwa hao nane na wanatarajia jitihada zao zitafanikiwa katika mchakato wa kusaka amani.

Aidha, kiongozi huyo amesema wanatarajia Uturuki pia itamuachia kiongozi wao Abdullah Ocalan kwani bila kufanya hivyo mchakato wa amani kati yao hautafanikiwa.

Uturuki bado haijatangaza itafanya nini kwa upande wao baada ya kuachwa huru kwa watu wao, lakini kumekuwepo na tetesi kuwa itafanya mabadiliko katika vipengele vya Katiba ya Uturuki ikiwemo kuitambua jamiii ya kikurdi, kama ambavyo jamii hiyo imekuwa ikidai.

PKK inataka kuachiliwa kwa mamia kwa maelfu ya wanasiasa na wanaharakati wake waliowekwa kizuizini kwa makosa ya kujihusisha na PKK.