SYRIA

Syria waadhimisha miaka miwili tangu kuanza harakati za kuuangusha utawala wa Rais Bashar al-Assad

uncyclopedia.wikia.com

Raia nchini Syria wanadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa harakati za upinzani kutaka kuipindua serikali ya Rais Bashar al-Assad. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa UN machafuko hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu sabini na maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani nchini humo umeendelea kusisitiza kuwa ni sharti Rais Assad andoke madarakani kwa kile wanachokisema uongozi wake umeendelea kugandamiza raia wa nchi hiyo.

Kwa upande wake Rais Assad ameendelea kusisistiza kuwa hawezi kujizulu na kushutumu mataifa ya Magharibi kuendelea kuwasaidia waasi nchini humo.

Wakati wa maadhimisho haya viongozi wa Ufaransa na Uingereza wanakutana mjini Brussels Ubelgiji kuwashinikiza wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya EU kuwasaidia wapinzani wa Syria kwa silaha.

Tayari Ufaransa imejiunga na Uingereza na kueleza wazi uamuzi wake wa kupeleka silaha kwa waasi wa Syria ikiwa hawatofanikiwa kuwashawishi wanachama wenzao wa EU kuondoa vikwazo vya silaha kwa wakati huu.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema lengo lao ni kuhakikisha wanafanikiwa kuishawishi EU na kama hawatafanikiwa badi Ufaransa itachukua jukumu hilo ili kukomesha umwagaji damu nchini Syria.

Akiongea baada ya kumalizika kwa siku ya kwanza ya mkutano huo Hollande amesisitiza kuwa suluhu ya kisiasa imeshindikana nchini Syria licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika hivyo wanatakiwa kutumia njia nyingine itakayomaliza machafuko hayo.

Mapambano ya kuuangusha utawala wa Rais Bashar al-Assad yalianza mwezi machi 2011.