OSCE-URUSI-Ushirikiano

Ukraine: hali ya taharuki yaendelea kutanda

Hali ya taharuki inaendeklea kutanda katika mji wa Odessa, ambao umeshuhudiwa kwa mara ya kwanza makabiliano na machafuko yaliyosababisha vifo vya watu tangu siku ya ijumaa hadi jana jumapili, wakati waasi wanaounga mkono Urusi wameshambulia makao makuu ya polisi na kuwatorosha wenzao waliyokua wameziwiliwa.

Waasi wanaounga mkono Urusi wakishambulia makao makuu ya polisi katika mji wa Odessa, Mei 4 mwaka 2014.
Waasi wanaounga mkono Urusi wakishambulia makao makuu ya polisi katika mji wa Odessa, Mei 4 mwaka 2014. REUTERS/Gleb Garanich
Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo, jeshi la Ukraine limekua likijaribu kuweka kwenye himaya yao maeneo yaliyoshikiliwa na waasi wanaounga mkono Urusi.

Hapo jana pia waziri mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk alikuwa mjini Odesa kuhudhuria mazishi ya watu 42 waliopoteza maisha kwenye ajali ya moto mwishoni mwa juma lililopita ambapo ametupia lawama vyombo vya usalama kwa kushindwa kuzuia mauaji hayo.

Hali ya machafuko katika mji wa Odessa, mei  4 mwaka 2014.
Hali ya machafuko katika mji wa Odessa, mei 4 mwaka 2014. REUTERS/Gleb Garanich

Utawala wa Ukraine unailaumu serikali ya Urusi kwa kuendelea kuwafadhili kwa silaha wafuasi wanaoiunga mkono hali ambayo utawala huo unasema inazidi kuchochea vurugu mashariki mwa nchi hiyo.

Hayo yakijiri, mkuu wa taasisi ya masuala ya usalama na ushirikiano wa Umoja wa Ulaya OSCE, Didier Burkhalter siku ya Jumatano anatarajiwa kufanya ziara nchini Urusi kukutana na rais Vladmir Putin, ziara inayolenga kujaribu kuishawishi nchi hiyo kumaliza machafuko mashariki mwa nchi ya Ukraine.