UKRAINE-Mapigano

Ukraine yapoteza wanajeshi katika mapigano na waasi

Mwanajeshi wa Ukraine,akiwa kwenye eneo liliyokaribu na mji wa lovyansk,mashariki mwa Ukraine.
Mwanajeshi wa Ukraine,akiwa kwenye eneo liliyokaribu na mji wa lovyansk,mashariki mwa Ukraine. REUTERS/Baz Ratner

Jeshi la Ukraine limepata hasara kubwa kufuatia operesheni yake dhidi ya wapiganaji wenye silaha wanaoiunga mkono Serikali ya Urusi mashariki mwa nchi hiyo ambapo ndege yake moja ya kijeshi na askari kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya Serikali inasema kuwa wanajeshi wanne wa Ukraine wameuawa kwenye mapigano hayo huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa kufuatia makabiliano kati yake na wapiganaji wenye silaha wanaodaiwa kusaidiwa na wanajeshi wa Urusi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine, Arsen Avakov, ametangaza leo jumanne kwamba “zaidi ya waasi 30 wanaunga mkono Urusi na wanajeshi 4 wameuawa katika mapigano yanayoendelea katika eneo la Slovyansk.

“Kwa mujibu wa takwimu zetu, zaidi ya magaidi 30 wameuawa na makumi wengine wamejeruhiwa”, ameandika waziri huyo kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook. Arsen Avakov amebaini kwamba miongoni mwa waasi hao wengi ni kutoka katika eneo la Crimea na Urusi, na wengine kutoka Chechenia. Waziri huyo amefahamisha pia kwamba wanajeshi 4 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, amesema kuwa operesheni hiyo imekuwa ngumu kutokana na kuwa wapiganaji hao wanatumia raia kama kinga dhidi ya mashambulizi yao.

Waasi wa Ukraine wanaounga mkono serikali ya Urusi  katika mji wa SLoviyansk, mashariki mwa Ukraine.
Waasi wa Ukraine wanaounga mkono serikali ya Urusi katika mji wa SLoviyansk, mashariki mwa Ukraine. REUTERS/Yevgeny Volokin

Mapigano haya yanazuka wakati huu Umoja wa Ulaya na Marekani zikiendelea na juhudi za kujaribu kuishawishi nchi ya Urusi kuingilia kati mzozo huo ambao unadaiwa kuchochewa na nchi hiyo.