UKRAINE-URUSI-Machafuko

Waasi wa Ukraine waitisha kura ya maoni

Denis Pouchiline (katikati),mmoja kati ya viongozi wa jamhuri ya watu waliyojitangaza ya Donetsk, akilakiwa na wafuasi wake katika mji wa Donetsk, mei 8 mwaka 2014.
Denis Pouchiline (katikati),mmoja kati ya viongozi wa jamhuri ya watu waliyojitangaza ya Donetsk, akilakiwa na wafuasi wake katika mji wa Donetsk, mei 8 mwaka 2014. REUTERS/Marko Djurica

Waasi wa Ukraine waanaounga mkono Urusi wameamua kubaki na msimamo wao wa kupiga kura jumapili ya uhuru wa eneo la mashariki mwa Ukraine, huku serikali ya Kiev ikitangaza kuendeleza operesheni ya kijeshi mashariki mwa taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Waasi hao wamepinga wito uliyotolewa na rais wa Urusi, Vladimir Putine ya kutaka kura hio ya maoni iahirishwe.

“Mkutano uliyoitishwa jumapili mashariki mwa Ukraine ili kutangaza uhuru wa jamhuri iliyojitenga ya Donetsk utafanyika kwa hali na mali mei 11”, wametangaza viongozi wa mji wa Donetsk na Slavyansk.

“Tarehe ya kupiga kura ya maoni kuhusu uhuru wa eneo la mashariki mwa Ukraine haitoahirishwa”, amesema Denis Pouchiline, mmoja kati ya viongozi wa eneo liliyojitenga, akibaini kwamba, baraza la waasi limependekeza tarehe hio mapema leo asubuhi.

Uamzi kama huo umeidhinishwa katika mkoa jirani wa Lugansk, kituo cha Interfax kimearifu.

“Zoezi hilo litasababisha hali inakua tata zaidi nchini Ukraine”, amesema msemaji wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, baada ya waasi kutoa tangazo hilo.

Hali ya makabiliano ikiendelea mashariki mwa Ukraine kati ya waasi na polisi ikishirikiana na jeshi.
Hali ya makabiliano ikiendelea mashariki mwa Ukraine kati ya waasi na polisi ikishirikiana na jeshi. REUTERS/Gleb Garanich

Rais wa Urusi Vladimir Putine amewatolea wito waasi wa Ukraine kuahirisha zoezi hilo la kupiga kura ya kuhusu uhuru wa eneo la mashariki, na kuwataka viongozi wa Kiev kusitisha opereshini ya kijeshi inayoendelea mashariki mwa Ukraine.

Waziri mkuu wa Ukraine Arseni Iatseniouk ametoa msimamo wake na kubaini kwamba rais Putine hana nia yoyote ya kushawishi waasi wasitishe mpango wao wa kutangaza kujitenga kwa maeneo ya mashariki mwa Ukraine, huku akibaini kwamba rais huyo wa Urusi ndiye chanzo cha kujitenga kwa maeneo hayo.

Ikulu ya Urusi ilifahamisha juma hili kwamba haina uwezo wa kushawishi waasi wa Ukraine kutokana na hali ambayo inaendelea kuwa mbaya zaidi mashariki mwa Ukraine.