ISRAEL-PALESTINA

Palestina kulalamika UNSC kuhusu ujenzi mpya wa makazi ya kudumu ya Israel

Ujenzi wa makazi ya walowezi wa Israel unaolalamikiwa na Palestina
Ujenzi wa makazi ya walowezi wa Israel unaolalamikiwa na Palestina eunews.it

Mamlaka ya Palestina hii leo imesema kuwa itakata rufaa kwenye baraza la Umoja wa Mataifa kupinga tangazo la Israel kuongeza ujenzi wa makazi mapya ya walowezi wa kiyahudi zaidi ya 1500, hatua inayokuja kufuatia muungano wa kundi la Hamas na chama cha PLO cha rais Mahamoud Abbas.

Matangazo ya kibiashara

Serikali mpya ya Palestina chini ya muungano wa vyama hivyo, inaungwa mkono na nchi ya Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, huku utawala wa Israel ukiendelea kusisitiza kutoitambua Serikali hiyo.

Mpango wa Israel kuongeza ujenzi wa makazi mapya ya walowezi ulitangazwa usiku wa kuamkia leo na waziri wa makazi wa taifa hilo ambaye amesema ujenzi huo umetokana na uamuzi wa kundi la Hamas na Fattah kuuungana na kumaliza tofauti zakimadaraka kati ya ukingo wa magharibi na Gaza.

Viongozi wa kundi la Hamas na Fattah wakizungumza baada ya kukubaliana kuunda Serikali ya pamoja hivi karibuni
Viongozi wa kundi la Hamas na Fattah wakizungumza baada ya kukubaliana kuunda Serikali ya pamoja hivi karibuni REUTERS/Mohammed Salem

Tangazo hili la ujenzi wa makazi mapya limelaaniwa vikali na Jumuiya ya Kimataifa ambayo inaona kuwa bado kulikuwa na nafasi ya mazungumzo kati ya Israel na mamlaka ya Palestina ili kufikia suluhu ya mzozo uliopo kati yao.

Uamuzi huu wa Israel umeamsha hasira kali toka kwa utawala wa Palestina ambao sasa umesema utakata rufaa kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupinga hatua hii mpya ya Israel.

Kwenye ujenzi huu mpya wa Israel, nyumba mia nne zitakuwa ni za walowezi waliohama toka kwenye ukingo wa Jerusalem na nyumba nyingine zitajengwa kwenye ukanda wa magharibi.

Akitangaza uamuzi huo, waziri wa nyumba wa Israel, Uri Ariel anasema "Nakaribisha uamuizi wa kuwapatia nyumba walowezi wa kiyahudi kama njia mojawapo ya kujibu kile kilichofanywa na serikali ya Kigaidi ya Palestina na kwamba huu ni mwanzo tu". Alisema Uri.

Afisa mmoja wa juu wa chama cha PLO, Hanan Ashrawi amesema kuwa nchi yake itawasilisha malalamiko yake kwenye baraza la usalama kutaka liingilie kati na kuiwajibisha Israel kutokana na kuendelea kupanua ujenzi wake wa makazi ya kudumu.

Ashrawi anasema "kamati kuu ya chama cha PLO inaona mpango huu wa Israel kama uchokozi na inachukua jambo hili kwa umakini mkubwa na utalieleza kwenye baraza la usalama na baraza kuu kama njia sahihi ya kukashifu uvamizi huu na kuonesha uwajibikaji". Aliongeza Ashrawi.