D-DAY

Viongozi wa dunia waungana kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 ya vita vya D-Day

Prince Charles wa Uingereza akisalimiana na sehemu ya wanajeshi waliopigana kwenye vita ya mwaka 1944 nchini Ufaransa.
Prince Charles wa Uingereza akisalimiana na sehemu ya wanajeshi waliopigana kwenye vita ya mwaka 1944 nchini Ufaransa. Reuters

Viongozi wa dunia hii leo wanakutana nchini Ufaransa, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 toka vita iliyotambulika kama D-Day, vita iliyopelekea taifa la Ufaransa kuwa huru na kumalizika kwa vita ya pili ya dunia. 

Matangazo ya kibiashara

Sherehe hizi zinafanyika kaskazini mwa nchi ya Ufaransa ambako operesheni kubwa ya majini ilifanyika mwaka 1944, marais, wafalme na malkia, mawaziri wakuu ni miongoni mwa viongozi watakaojumuika pamoja na wanajeshi waluiopigana kwenye vita hiyo ambao sasa wamefikisha umri wa miaka 90.

Miongoni mwa wageni maalumu kwenye sherehe hizi ni pamoja na Malikia Elizabeth wa pili wa Uingereza, ambaye akiwa na umri wa miaka 88 hivi sasa hii inakuwa ni ziara yake ya nadra kufanya nje ya taifa la Uingereza.

Sherehe hizi zinafanyika huku viongozi wa Ulaya wakitarajiwa kutumia maadhimisho haya kueleza umuhimu wa operesheni iliyofanyika mwaka 1944 na kulikomboa eneo la Ulaya pamoja na kumueleza rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusu uvamizi wake kwenye nchi ya Ukraine.

Rais wa Marekani Barack Obama, waziri mkuu wa Uingereza, David Cameroon, Kansela wa Ujerumani, Angela Markel watakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na rais wa Urusi, Vladmir Putin kumueleza kutoridhishwa kwao na uvamizi wa nchi yake kwa nchi ya Ukraine.

Sehemu ya makaburi ambako wamezikwa wanajeshi waliopigana wakati wa vita vya D-Day
Sehemu ya makaburi ambako wamezikwa wanajeshi waliopigana wakati wa vita vya D-Day REUTERS/Pascal Rossignol/Files

Zaidi ya wapiganaji 1800 walioshiriki kwenye vita hivyo toka kwenye nchi za Marekani, Uingereza, Ufarasa, Canada, Urusi na Poland watatunukiwa tuzo maalumu kutambua mchango wao na kujitolea kwao wakati wa vita hivi vilivyomaliza vita ya pili ya dunia.

Vita ya D-Day kama inavyptambulika duniani, ilihusisha operesheni kubwa ya majini iliyowahusisha wanajeshi toka kwenye mataifa ya Ulaya na Amerika kupambana na wanajeshi wa Ujerumani waliokuwa chini ya utawala wa Kinazi na hatimaye kulikomboa eneo la Ulaya na Ulaya mashariki.

Viongozi wengi wanatarajiwa kutumia sherehe hizi kuelezana ukweli kuhusu mizozo mbalimbali inayoendelea kushuhudiwa duniani ikiwemo mzozo wa Syria na sasa Ukraine.