UINGEREZA-Siasa

Uingereza: waziri mwingine ajiuzulu

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye serikali yake inakabiliwa na wimbi la kujiuzulu kwa mawaziri.
Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye serikali yake inakabiliwa na wimbi la kujiuzulu kwa mawaziri. REUTERS/Olivia Harris

Serikali ya waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron imepata pigo jingine baada ya waziri wake anayehusika na masuala ya Afrika, Mark Simmonds kutangaza kujiuzulu nafasi yake, wiki moja baada ya waziri mwingine kujiuzulu kutokana na mzozo wa Israel.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa wa serikali ya Uingereza wamesema kuwa kujiuzulu kwa waziri Simmonds hakuna uhusiano wowote na hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri anayehusika na masuala ya kijamii, Sayeeda Warsi, aliyejiuzulu kwa kile alichosema ni sera mbovu za serikali katika kushughulikia mzozo wa Israel na Palestina.

Kwenye barua yake aliyomtumia waziri mkuu Cameron, waziri Simmonds amebainisha kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu hauna uhusiano wowote na sera ya serikali kuhusu mashariki ya kati na badala yake anataka kutumia muda mwingi na familia yake.

Waziri Simmonds ameongeza kuwa yeye ni mmoja kati ya viongozi wanaounga mkono sera zote za serikali ya Uingereza ikiwemo ile ya kushughulikia mzozo wa Israel na Palestina pamoja na sera nyingine za kimaendeleo.

Kujiuzulu kwa waziri Simmonds kumeelezwa kuwa ni pigo kwa waziri wa mambo ya kigeni Philip Hammond aliyechukua nafasi hiyo toka kwa William Hague aliyetangaza kujiuzulu majuma kadhaa yaliyopita na kufanya wizara hiyo kuwa na mawaziri wanne ambao wamedumu chini ya muda wa mwezi mmoja.