UKRAINE

Mataifa ya Magharibi yaitaka Urusi Kuthibitisha inataka amani nchini Ukraine

Viongozi wa mataifa ya Magharibi wamempa changamoto rais wa Urusi Vladimir Putin kuthibitisha kuwa anataka amani nchini Ukraine, na kuonya pande zote mbili kuwa mchakato wa amani unaofanywa na Ujerumani na Ufaransa huenda ikawa nafasi ya mwisho kumaliza mzozo huo.

Rais Ukraine Poroshenko aonyesha paspoti na vitambulisho vya uraia ili kuthibitisha uwepo wa majeshi ya Urusi nchini Ukraine, katika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama, Munich tarehe 7 Februari mwaka 2015.
Rais Ukraine Poroshenko aonyesha paspoti na vitambulisho vya uraia ili kuthibitisha uwepo wa majeshi ya Urusi nchini Ukraine, katika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama, Munich tarehe 7 Februari mwaka 2015. REUTERS/Michael Dalder
Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano huo mkubwa wa viongozi wa dunia nchini Ujerumani, Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alionesha hati za kusafiria na vitambulisho vya kijeshi akisema vilikamatwa kutoka kwa askari wa Urusi ndani ya nchi yake,huo ukiwa ushahidi wa uwepo wa Urusi katika nchi hiyo.

Kwa upande wa Marekani Makamu wa rais , Joe Biden, amesema Marekani iko tayari kuisaidia Ukraine kujihami dhidi ya wapiganaji wanaosaidiwa na Urusi ili kupata suhulu ya amani nchini Ukraine.

Hata hivyo Biden amesema mara nyingi rais Putin ameahidi amani huku akiendelea kuwapatia wapiganaji wanajeshi, vifaru na silaha.

Hapo awali, kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel, alionya kuwa Ukraine isipatiwe silaha na kusisitiza kuwa hakuna hakika kuwa juhudi za sasa za kutafuta amani zitafanikiwa.

Rais Putin amekanusha kuwa Urusi inataka vita lakini kwa mara nyigine tena amelalamika juu ya vikwazo vilivowekwa na mataifa ya magharibi dhidi ya nchi yake.