UFARANSA-USALAMA-

Manuel Valls ziarani Marseille

Waziri Mkuu Manuel Valls na Waziri wa Mambo ya Ndani Bernard Cazeneuve, katika mji wa Marseille, Februari 9 mwaka 2015.
Waziri Mkuu Manuel Valls na Waziri wa Mambo ya Ndani Bernard Cazeneuve, katika mji wa Marseille, Februari 9 mwaka 2015. REUTERS/Jean-Paul Pelissier

Watu waliojificha nyuso wakiwa na silaha walishambulia kwa risasi gari ya polisi katika mji muhimu wa Marseille, nchini Ufaransa, Jumatatu wiki hii, masaa machache kabla ya kuwasili kwa Waziri mkuu Manuel Valls, ambaye alikuja kupongeza kupungua kwa uhalifu katika mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Pierre-Marie Bourniquel, mkurugenzi wa Idara ya usalama wa umma katika eneo la Bouches-du-Rhône, alikua katika gari hiyo ya polisi, ambaye alitumwa baada ya wakazi wa mji wa Marseille kupigia simu polisi wakiitarifu kuwepo kwa watu waliojificha nyuso wakiwa na silaha. Gari hiyo ya polisi ilishambuliwa kwa risasi, lakini bila hata hivyo kumjeruhi mkurugenzi huyo.

Kikosi cha polisi kilitumwa katika kata ya Castellane, ambapo milio ya risasi ilisikika, huku vikosi vya usalama vikizingira barabara zinazoingia na kutoka katika mji huo unaopatikana katika maeneo ya kaskazini ya mji.

Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya ndani, Bernard Cazeneuve, ambaye alikua ameambatana na Manuel Valls katika mji wa Marseille, bunduki 7 aina ya Kalachnikov na kilo kadhaa za madawa ya kulevya vilikamatwa. Vipimo na vinasaba vingine vinafanyiwa uchunguzi ili kuwakamata wahusika, amesema Bernard Cazeneuve.

Wakazi 7,000 wa mji huo walitakiwa kwa masaa kadhaa kusalia nyumbani, huku wanafunzi wakitakiwa pia kusalia katika shule zao.

Waziri mkuu amesema katika hotuba yake mbele ya vikosi vya usalama vya mji wa Marseille kwamba “ kuvalia tu sare bila kibali chochote“ ni kuitia polisi hatarinii.