UKRAINE-UFARANSA-UJERUMANi-URUSI-AMANI-USALAMA

Vladimir Putin: " Tumefikia mkutano wa amani kuhusu Ukraine"

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amehakikishia vyombo vya habari baada ya mkutano wa amani mjini Minsk, kwamba wamefikia mkataba wa amani kuhusu Ukraine.

Kutoka kushoto kwenda kulia, rais wa Belarusi, Alexander Lukashenko na viongzi wanne Vladimir Putin, Angela Merkel, François Hollande na Petro Poroshenko, Jumatano Februari 11 mwaka 2015.
Kutoka kushoto kwenda kulia, rais wa Belarusi, Alexander Lukashenko na viongzi wanne Vladimir Putin, Angela Merkel, François Hollande na Petro Poroshenko, Jumatano Februari 11 mwaka 2015. REUTERS/Grigory Dukor
Matangazo ya kibiashara

Vladimir putin, amebaini kwamba mkutano huo unahusu masuala mawili nyeti: usitishwaji mapigano kuanzia Februari 15, pamoja na kuondoa silaha za kivita mashariki mwa Ukraine.

" Tumefanikiwa kufikia mkataba kuhusu masuala nyeti", amesema rais wa Urusi katika mkutano wa amani kuhusu Ukraine unaofanyika katika mji mkuu wa Belarusi, Minsk. Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Ukraine wanakutana tangu Jumatano wiki hii mjini Minsk, kujaribu kutafutia suluhu machafuko yanayoendelea Ukraine.

Hayo yanajiri wakati mapigano kati ya jeshi la ukraine na waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki yanaendelea kushika kasi kila kukicha. Mtu mmoj aliuawa Jumatano katika mashambulizi karibu na hospitali ya mjini Donetsk.

Duru kutoka Ukraine zilikua zinafahamisha kwamba viongozi katika mkutano huo Jumatano usiku wiki hii walikua wanatazamiwa kutia saini katika tangazo la pamoja ya kuunga mkono uhuru wa Ukraine.

Rais Alexandre Loukachenko, ambae anachukuliwa kama dikteta barani Ulaya, amewapokea viongozi wa Urusi na Ukraine, na vile vile François Hollande na Angela Merkel. Ni kwa mara ya kwanza tangu miaka 76 iliyopita, kiongozi katika ngazi ya juu nchini Ujerumani kuingia katika mji wa Minsk, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu katika utawala wa Georges Pompidou mwaka 1973, rais wa Ufaransa akijielekeza katika mji huo wa Minsk.

Rais wa Ufaransa, François Hollande, amesema juhudi za kidiplomasia zinaendelea kuzuia Ukraine kutumbukia katika dimbwi la machafuko.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI Minsk, Muriel Pomponne, Jumatano jioni wiki hii, baada ya saa moja na nusu ya mkutano, mazungumzo yaliendelea kwa upana yakiwajumuisha wajumbe mbalimbali kutoka mataifa hayo yanayochangia ili amani ya kudumu ipatikane nchini Ukraine. Viongozi hao wanne pamoja na washauri wao walikua wakijadili stakabadhi ziliyoandaliwa kwa siku kadha na wanadiplomasia wao.

Hayo yakijiri, watu 47 waliuawa katika mapigano yaliyotokea Jumanne wiki hii. Rais wa Ukraine ametishia kuwa iwapo mazungumzo hayo yataambulia patupu, sheria ya kijeshi itatekelezwa katika nchi nzima ya Ukraine.