URUSI

Maandamano ya upinzani Urusi yageuka maandamano ya maombolezo

Maelfu ya watu wamejitokeza kutoa salamu za rambirambi wakiwa na mishumaa na maua katika eneo ambalo mwanasiasa wa upinzani nchini Urusi Boris Nemtsov aliuawa kwa kufyatuliwa risasi.

Waombolezaji wakiweka maua kuomboleza kifo cha  Boris Nemtsov nchini Urusi, Februari 28 mwaka 2015.
Waombolezaji wakiweka maua kuomboleza kifo cha Boris Nemtsov nchini Urusi, Februari 28 mwaka 2015. REUTERS/Sergei Karpukhin
Matangazo ya kibiashara

Maandamano ya upinzani yaliyopangwa kufanyika leo jumapili yamegeuka kuwa maandamano ya kumkumbuka kiongozi huyo Nemtsov.

Raisi Vladimir Putin wa Urusi amelaani na kuyaita mauaji hayo ya kinyonge na kijinga huku akiahidi kuwabaini wauaji.

Hata hivyo washirika wa Nemtsov walisema kwamba mauaji haya ni ya kisiasa yalihusishwa na upinzani kwa raisi Putin na mzozo wa Ukraine.

Viongozi wa mataifa ya magharibi na upinzani nchini Urusi zimelaani mauaji ya mkosoaji wa serikali ya Urusi Boris Nemtsov wakati raisi Vladimir Putin akisema kwamba uhalifu huo ulipangwa kwa lengo la kuiletea tuhuma serikali yake.

Naye Raisi wa Marekani Barack Obama amelaani mauaji tata na ya kikatili ya Nemtsov,ambayo yamesababisha kuahirishwa kwa maandamano makubwa ya jumapili na kutoa wito kwa Urusi kuanza uchunguzi usio na upendeleo.

Kwa upande wake Raisi wa Ufaransa Francois Hollande ameyaita mauaji hayo mauaji ya chuki kwa mtetezi wa demokrasia huku waziri mkuu wa uingereza David Cameron akisema mauaji hayo ya kikatili lazima yachunguzwe mara moja kwa uwazi na haraka.