IRAN-MAREKANI-UFARANSA-URUSI-CHINA-UJERUMANI-UINGEREZA-NYUKLIA-DIPLOMASIA

Mpango wa nyuklia wa Iran: muda wa mwisho watamatika

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius ameondoka Lausanne usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano Aprili 1 mwaka 2015.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius ameondoka Lausanne usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano Aprili 1 mwaka 2015. REUTERS/Brendan Smialowski/Pool

Mazungumzo kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran yataendelea Jumatano mjini Lausanne, hata kama tarehe ya mwisho ya Machi 31 imetamatika.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe wengi wamethibitisha Jumanne Jioni wiki hii kwamba hatua kubwa imepigwa kwa kuendelea na mazungumzo na kujaribu kutafutia suluhu matatizo yanayosalia, lakini bado kuna mkanganyiko. Upande wa Ufaransa, bado hawajawa na matumaini.

Kwa mujibu wa mwanahabari wa RFI mjini Lausanne, Sami Boukhelifa , Jumanne wiki hii mazungumzo yaliendelea katika mji wa Lausanne bila hata hivyo kupumzika. Lakini bado kumeendelea kushuhudiwa mvutano katika mazungumzo hayo. Ufaransa kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Laurent Fabius, imesema itainyooshea Iran kidole ccha lawama endapo mazungumzo hayo yatagonga mwamba.

Wakati huohuo Laurent Fabius aliondoka ghafla katika ukumbi wa Beau-Rivage Palace kunakofanyika mazungumzo hayo. Duru za kuaminika, kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, Laurent Fabius alieleza kinagaubaga. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema muda wa mwisho haukuwekwa kwa kuwachanganya wajumbe wanaoshiriki katika mazungumzo hayo.

“Tarehe 31 Machi na Aprili 1 ni siku mbili tafauti, kwa hiyo hatupaswi kuendelea kuongeza siku ili tupoteze muda, wakati hakuna kinacho tarajiwa kufikiwa”, amesema Laurent Fabius.

Hata hivyo ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo umesema hatua kubwa zimefikiwa. Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, amesema ana matumaini kwamba mazungumzo hayo yatamalizika Jumatano wiki hii.

Upande wa Marekani, kupitia wajumbe wake wanaoshiriki katika mazungumzo hayo imebaini kwamba kuna masuala ambayo yalikua hayajapatiwa suluhu.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergueï Lavrov, alisema hivi karibuni kwamba mataifa yenye nguvu pamoja na Iran walikua wamefikia makubaliano ya kanuni kuhusu masuala nyeti ya mpango wa Nyuklia wa Iran.