ARANSA-FN-SIASA

Marine Le Pen aanzisha utaratibu wa kinidhamu dhidi ya baba yake

Kiongozi wa chama cha FN (National Front), Marine Le Pen, akialikwa na runinga ya TF1 katika taarifa ya habari ya Alhamisi jioni Aprili 9 mwaka 2015.
Kiongozi wa chama cha FN (National Front), Marine Le Pen, akialikwa na runinga ya TF1 katika taarifa ya habari ya Alhamisi jioni Aprili 9 mwaka 2015. REUTERS/Martin Bureau/Pool

Chama cha FN kinakabiliwa wakati huu na malumbano ya ndani, baada ya kuibuka mvutano kati ya kiongozi wa chama cha FN, Marine Le Pen na baba yake, Jean-Marie Le Pen, ambaye ni mwanziishi wa chama hicho.

Matangazo ya kibiashara

Akialikwa na runinga ya TF1 Alhamisi usiku wiki hii katika taarifa ya habari ya jioni, kiongozi wa chama cha FN, Marine Le Pen ametangaza uamuzi wake wa kuanzisha utaratibu wa kinidhamu dhidi ya baba yake Jean-Marie Le Pen na kumtaka kustaafu kutoka kwenye siasa kutokana na chokochoko zake za mara kwa mara.

Malumbano haya ya kisiasa katika chama cha FN yaliibuka kutokana na matamshi ya mwanzilishi wa chama hicho katika gazeti la kila wiki linaloegemea mrengo wa kulia la Rivarol.

" Kama tungeliweza kuachana na mgogoro huu, ingelikua ni furaha kwetu", amesema Marine Le Pen katika kanda ya kifaransa ya runinga ya TF1. Pia amezungumza kuhusu " huzuni wake kama binti"  dhidi ya " kauli zisiyokubalika" za baba yake, kabla ya kuweka wazi jukumu lake kama kiongozi wa chama cha FN : " Kabla ya yote, sisi ni viongozi wa kisiasa ", amesema Marine Le Pen, kabla ya kutangaza kwamba baba yake hivi karibuni ataitishwa kama sehemu ya "utaratibu wa kinidhamu" mbele ya kamati ya utendaji ya chama, lakini bila kufafanua ni vikwazo vipi ambavyo anaweza kuchukuliwa.

Hata hivyo, Marine Le Pen amethibitisha kwamba amepinga jina la baba yake kuwekwa kwenye mstari wa mbele kwenye orodha ya watakaogombea katika uchaguzi wa mikoa kwa tiketi ya chama cha FN, hususan katika mkoa wa Provence-Alpes-Côte d'Azur.

" Baba yangu hana ushawishi mkubwa katika uchaguzi huu ", amesema Marine Le Pen, kabla ya kuombi baba yake aondolewe katika ukumbi wa siasa.

" Jean-Marie Le Pen anapaswa kuwa na hekima, kufuatia vurugu alizosababisha na kuacha majukumu yake ya kisiasa ", Marine Le Pen ameongeza.

Ujumbe bila suluhu ya msichana kwa baba yake. Mazingira ambayo yataepusha uwezekano wa kutengwa, iwapo Jean-Marie Le Pen atakubaliana na fikra hii ya kuachana na siasa.