UGIRIKI-DENI-ULAYA

Tsipras: Wananchi wa Ugiriki pigeni kura ya hapana kukataa matakwa ya wakopeshaji

Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras REUTERS/Alkis Konstantinidis

Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras ametoa wito kwa wananchi wake kupiga kura ya hapana mwishoni mwa juma hili ili kukataa matakwa ya wakopeshaji, wakati huu nchi hiyo ikishindwa kulipa deni lake kwa shirika la fedha duniani IMF. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri mkuu Tsipras amesema kuwa iwapo wananchi watapiga kura ya hapana kupinga mpango wa ubanaji matumizi na matakwa ya wakopeshaji wa kimataifa basi nchi yake itakuwa kwenye nafasi nzuri ya mazungumzo na viongozi wa Ulaya.

Katika kile kinachoonekana kuwa amechukizwa na namna ambavyo viongozi wa Ulaya wanashughulikia tatizo la nchi yake, waziri mkuu Tsipras amesema kuwa iwapo wananchi wataamua vinginevyo basi hatakuwa tayari kuendelea kukaa ofisini huku akishuhudia mpango huu ukiendelea kuwamiza wananchi.

Muda wa mwisho wa Ugiriki kuweza kujinasua kwenye mzozo wa ulipaji mkopo wake na kusaidiwa kifedha unaisha hii leo wakati huohuo leo ndio siku ya mwisho kwa nchi hiyo kutakiwa kulipa mkopo wa kiasi cha Euro bilioni 1.1 kwa shirika la fedha duniani IMF.

Ugiriki inapaswa kuwa imelipa deni lake kwa IMF ifikapo saa kumi na mbili kamili za jioni ya leo kwa saa za Washington.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameonya kuwa iwapo wananchi wa Ugiriki watapiga kura ya hapana kukataa matakwa ya wakopeshaji wa kimataifa, hatua hiyo itakuwa inamaanisha kuwa Ugiriki inajitoa kwenye Ukanda wa Ulaya, jambo ambalo waziri mkuu Tsipras anasema asingependa litokee.

Mazungumzo kati ya Ugiriki, wakopeshaji na viongozi wa Ulaya yalivunjika juma moja lililopita hali ambayo mwishoni mwa juma Serikali ya Ugiriki imetangaza kuzifunga benki zake zote na kuweka masharti utoaji fedha kwenye mashine za ATM.

Hata hivyo licha ya changamoto zinazoikabili nchini ya Ugiriki, waziri mkuu Tsipras ameonesha nia ya kuwa tayari kuendelea na mazungumzo na viongozi wa Ulaya ambao nao wameonesha utayari wa kuwa na mazungumzo mengine na utawala wa Athens kuinusuru nchi hiyo kufilisika.