UHISPANIA-SYRIA-WANAHABARI-USALAMA

Wanahabari watatu wa Uhispania watoweka Syria

Waandishi wa habari watatu waliingia Syria Julai 10 wakipitia Uturuki na walielekea Aleppo ( kwenye picha).
Waandishi wa habari watatu waliingia Syria Julai 10 wakipitia Uturuki na walielekea Aleppo ( kwenye picha). REUTERS/Abdalrhman Ismail

Waandishi wa habari watatu wa Uhispania wametoweka nchini Syria tangu siku kumi zilizopita. Antonio Pampliega, Jose Manuel Lopez na Angel Sastre waliwasili nchini Syria Julai 10 na hawajatoa taarifa yoyote tangu Julai 12, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Shirikisho la waandishi wa habari nchini Uhispania, Elsa Gonzalez, akizungumza kwenye televisheni ya serikali ya Uhispania TVE 24.

Matangazo ya kibiashara

Vyanzo vilio karibu na serikali ya Syria na upinzani katika mji wa Beirut vilivyowasiliana na RFI, vimebaini kwamba kuna uwezekano kuwa waandishi hao wa habari walitekwa nyara.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, mjini Beyrut, Paul Khalifeh, wanahabri hao wa Uhispania waliingia Syria wakitokea Uturuki na kuelekea kwenye mji wa Aleppo, kaskazini-magharibi mwa Syria. Julai 12, siku ambayo walitoweka, walikuwa katika eneo la mapigano ambapo makundi ya wanamgambo wa kiislamu yanayojumuika katika muungano unaojulikana kama Ansar Al-Shariah huwa yakiendeshea harakati zao.

Muungano mwengine unaojulikana kama Fatah Halab, ambao unamaanisha kwa Kiarabu "ushindi wa Aleppo", pia una ushawishi mkubwa katika eneo hilo. Muungano huu unaundwa na makundi mengi, ikiwa ni pamoja na Al-Nusra Front, tawi la al Qaeda nchini Syria.

Elsa Gonzalez,mwenyekiti wa Shirikisho la waandishi wa habari nchini Uhispania, hajabaini iwapo wanahabari hawa watatu binafsi walikuwa pamoja, na wanafanya kazi kwa vyombo gani vya habari. Antonio Pampliega alichangia kupeperusha habari kwa shirika la habari la Ufaransa (AFP) nchini Syria mpaka mwaka 2013. Jose Manuel Lopez alishiriki kwa kulirushia shirika la habari la Ufaransa (AFP) picha za migogoro mingi, ikiwa ni pamoja na migogoronchini Syria hadi mwaka 2013 , limebaini shirika hilo. Televisheni ya serikali ya Uhispania imesema kwa upande wake kuwa imekua ikiendesha pamoja na wanahabari hao uchunguzi nchini Syria.

Tangu kuanza kwa mgogoro nchini Syria, mwaka 2011, mamia ya waandishi wa habari wa Syria na wengine kutoka nchi za kigeni walitekwa nyara au waliuawa. Miongoni mwao ni Wahispania watatu, Javier Espinosa, Ricardo Garcia Vilanova na Marc Marginedas, walioachiliwa huru mwezi Machi mwaka 2014 na kundi la Islamic State, baada ya miezi wakishikiliwa. Waandishi wa habari wengi walitekwa na makundi mengine ya wanamgambo wa kiislamu kabla ya kuuzwa au kufikishwa mikononi Islamic State.