AFGHANISTAN-UJERUMANI-TALIBAN-USALAMA

Afghanistan: raia wa Ujerumani atekwa nyara Kabul

Nchini Afghanistan, Jumatatu asubuhi wiki hii, mfanyakazi wa shirika la kihisani kutoka Ujerumani alitekwa nyara na watu wenye silaha wasiojulikana wakati aliondoka nyumbani kwake akielekea kazini.

Askari polisi wa Afghanistan akitoa ulinzi katika kituo cha ukaguzi mjini Kabul, Agosti 17, 2015, wakati ambapo mfanyakazi wa shirika la kihisani kutoka Ujerumanialitekwa nyara na watu wasiojulikana baada ya kumpitisha kwenye dirisha la gari lake.
Askari polisi wa Afghanistan akitoa ulinzi katika kituo cha ukaguzi mjini Kabul, Agosti 17, 2015, wakati ambapo mfanyakazi wa shirika la kihisani kutoka Ujerumanialitekwa nyara na watu wasiojulikana baada ya kumpitisha kwenye dirisha la gari lake. REUTERS/Omar Sobhani
Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo linatokea baada ya mashambulizi kadhaa kushuhudiwa katika mji mkuu wa Afghanistan tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI katika mji wa Kabul, Joël Bronner, tukio hili lilitokea katika mji wa Taimani katikati mwa mji mkuu wa Afghanistan, ambapo mashirika mengi ya kimataifa ya kihisani yamepiga kambi. Mwanamke mmoja ambaye amekua akifanya kazi katika shirika kutoka Ujerumani la GIZ, alitekwa nyara baada ya kupitishwa kwenye dirisha la gari lake na watu wenye silaha.

Mfanyakazi mwingine wa shirika hili, linaloendesha shughuli zake nchini Afghanistan, alitekwa nyara katika mji wa Kunduz kaskazini mwa nchi hiyo mwezi Aprili, kabla ya kuachiliwa huru mwezi mmoja baadaye.

Tukio hili la utekaji nyaralinatokea wakati mji wa Kabul umeendelea kukabiliwa na wimbi la ghasia tangu wiki mbili zilizopita ikiwa ni pamoja na mashambulizi karibu na uwanja wa ndege na katika chuo cha polisi pamoja na mlipuko wa bomu lililotegwa katika lori. Hii ni mfululizo wa mashambulizi yaliowaua watu wengi katika mji mkuu wa Afghanistan tangu mwaka 2014. Mashambulizi haya yamekithiri baada ya majeshi ya NATO kuondoka nchini Afghanistan mwezi Desemba uliopita.

Machafuko ya sasa yamezuka katika kutafuta mrithi katika uongozi wa kundi la Taliban la Mullah Omar baada ya kifo chake kutangazwa rasmi na kuthibitishwa mwishoni mwa mwezi Julai. Nafasi yake ilichukuliwa na Mullah Mansour, lakini tangu wakati wakati kundi la taliban liligawanyika na kusababisha hali ya sintofahamu katika kundi hilo.