UFARANSA-LAGARDE-SHERIA

Sapin: "Lagarde bado hajakabiliwa na hatia"

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Christine Lagarde, anaweza kusalia kwenye wadhifa wake kwa sababu "hana hatia", Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Michel Sapin, amesema Alhamisi hii katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York.

Waziri wa Fedha wa Ufaransa Michel Sapin (kushoto) na mkurugenzi mkuu wa IMF, Christine Lagarde, Mei 28, 2015 katika mji wa Dresden, Ujerumani.
Waziri wa Fedha wa Ufaransa Michel Sapin (kushoto) na mkurugenzi mkuu wa IMF, Christine Lagarde, Mei 28, 2015 katika mji wa Dresden, Ujerumani. AFP/AFP
Matangazo ya kibiashara

Lagarde ametumwa mbele ya mahakama ya Ufaransa kwa madai ya kuhusika kwake katika kesi ya Mkopo kwa Bernard Tapie wakati alikuwa Waziri wa Uchumi nchini Ufaransa.

"Lagarde hana hatia, kwa hiyo sioni jinsi gani hali hii inaweza kumzuia kuendelea na majukumu yake ya sasa", Sapin amesema.

Waziri wa Fedha wa Ufaransa alikuwa mjini New York katika mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya ufadhili wa kundi la Islamic State.

"Sheria ya Ufaransa inaundwa kwa kanuni ya msingi kabisa, ambayo ni ile ya mtu kutokua na hatia kabla hajahukumiwa", Michel Sapin ameonya. "Christine Lagarde ananufaika na sheria hiyo".

"Hakuna sababu leo ya kubadili jambo lolote katika utendaji kazi wa majukumu yake. Ufaransa kama mwanachama wa bodi ya uongozi ya IMF inaamini kwamba Lagarde bado ana uwezo kamili wa kuendelea kutekeleza majukumu yake", amesema Waziri wa Fedha wa Ufaransa.

Alipoulizwa kama Ufaransa imepoteza nafasi kwenye uongozi wa IMF kwa sababu ya jambo hili, Michel Sapin amekumbusha kwamba "taasisi za IMF zitarejelewa upya. Ni katika wakati huo ambapo swali hilo litajitokeza", ameongeza Sapin.

Michel Sapin amekataa kutoa maoni yake kwa undani kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Jamhuri (CJR). Mahakama hii, amesema, "inafanya kazi yake, inafanya hivyo hadi mwisho na itafanya hivyo hadi mwisho bila maoni yoyote kutoka kwa mjumbe hata mmoja wa Serikali ya Ufaransa kuhusu kazi hii."

Kwa mujibu wa chanzo cha mahakama, CJR imeamuru kwamba Bi Lagarde atahukumiwa kwa uzembe katika usimamizi wa fedha za umma, kosa ambalo alifanyiwa uchunguzi katika majira ya joto mwaka 2014.

Kesi ilianza 2008 wakati Mahakama binafsi ya usuluhishi ilipitishwa na Wizara ya Uchumi, wakati huo ikiongozwa na Bi Lagarde, ilimpa Bernard tapie zaidi ya Euro milioni 404.

Bernard Tapie alikua akibaini kwamba akifanyiwa utapeli na benki ya Mkopo ya Lyon wakati mauzo ya kampuni ya Adidas mwaka 1994.