UHISPANIA-UCHAGUZI-SIASA

Uhispania: chama cha mrengo wa kulia chashinda uchaguzi

Wafuasi wa chama cha PP kwenye makao makuu ya chama mjini Madrid baada ya kutangazwa kwa matokeo, Jumapili, Desemba 20, 2015.
Wafuasi wa chama cha PP kwenye makao makuu ya chama mjini Madrid baada ya kutangazwa kwa matokeo, Jumapili, Desemba 20, 2015. REUTERS/Marcelo del Pozo

Chama tawala cha mrengo wa kulia nchini Uhispania kimeibuka mshindi wa uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumapili hii Desemba 20, kwa kupata 28.7% ya kura kulingana na matokeo ya zaidi ya 90% ya kura, zilizotangazwa na Makamu wa rais wa serikali Soraya Saenz Santamaria.

Matangazo ya kibiashara

"Kwa mujibu wa takwimu ambazo tunazo, pamoja na 90.39% ya kura zilizohesabiwa, chama tawala kimeshinda uchaguzi mkuu", Saenz Santamaria amesema, akibainisha kuwa chama cha kisoshalisti kinachukua nafasi ya pili kwa 22.19% ya kura. Chama cha Podemos cha mrengo wa kushoto chenye msimamo mkali kimechukua nafasi ya "tatu", Makamu wa rais wa serikali ameongeza.

Chama cha PP, madarakani tangu mwaka 2011 nchini Uhispania, kimeshinda uchaguzi. Lakini kimepoteza wingi wa viti, na hivyo Bunge litaundwa na vyama vyote viliopata kura za kutosha ambazo zitaviwezesha kushiriki katika Bunge.

Kwa mujibu wa matokeo, chama cha PP cha Mariano Rajoy kimepata wabunge 123 kwa jumla ya wabunge 350 wa Bunge la Uhispania, sawa na viti 63 ambavyo imepoteza ikilinganishwa na mwaka 2011, na hivyo kupoteza wingi wa viti Bungeni.

Chama cha PP kinafuatiwa na chama cha Kisoshalisti cha PSOE, ambacho kimepata wabunge 90, matokeo mabaya zaidi katika historia ya chama hicho.

Chama cha mrengo wa kushoto chenye msimamo mkali cha Podemos Pablo Iglesias, ambacho kina mwaka mmoja wa kuanzishwa kwake, kikishirikiana na washirika wake kimepata kwa jumla wabunge 69, na hivyo kuchukua nafasi ya tatu.

Chama cha Ciudadanos kimepata viti 40.