UINGEREZA-IS-VITISHO

Syria: IS yaitishia Uingereza na David Cameron katika video mpya ya mauaji

Wapiganaji wa kundi la IS wakimuonya David Cameron, Waziri mkuu wa Uingereza.
Wapiganaji wa kundi la IS wakimuonya David Cameron, Waziri mkuu wa Uingereza. Reuters

Kundi la Islamic State (IS) limeitishia Uingereza katika video mpya inayoonyesha mauaji ya raia watano ambao kundi hilo limewaita "wapelelezi".

Matangazo ya kibiashara

Video hii, iliorushwa hewani Jumapili hii kwenye mitandao ya makundi ya kiislamu na kuripotiwa na kituo cha Marekani kinachofuatilia mitandao ya makundi hayo, inaanza na "kukiri" mbele ya kamera kwa watu wanaodai kuwa ni wakazi wa Raqa, "mji mkuu" wa kundi la Islamic state, nchini Syria.

Watu hao wameonyeshwa na kundi hili la kigaidi kama "wapelelezi".

Kauli za watu hawa watano hazionyeshi taifa au mataifa ambayo wanatuhumiwa kufanyia upelelezi, lakini mmoja wao ameutaja muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, ambao unaendesha vita dhidi ya kundi la Islamic State katika nchi za Iraq na Syria.

Watu hao wanasema kuwa wamekua wakipiga picha au video zinazoonyesha hali ya maisha mjini Raqa kwa niaba ya watu wanaopiga kambi nchini Uturuki, au pia kuchunguza harakati za wapiganaji wa IS.

Katika video nyingine inaonyesha watu hao watano wakiwa wamevaa nguo za rangi ya ya machungwa wanaovaa wafungwa wa IS, wakipiga magoti mbele ya watu watano wanaoficha nyuso zao, ambao wote wamevaa sare za jeshi, huku wakishikilia bastola.

"Huu ni ujumbe kwa David Cameron, Waziri Mkuu wa Uingereza", mmoja wa wanamgambo hao wa IS anasema kwa Kiingereza: "Ni jambo la kushangaza kusikia leo kiongozi asioeleweka kama wewe anapinga nguvu za Islamic State".

Uingereza, ambayo imekua ikiendesha mashambulizi dhidi ya ngome za IS nchini Iraq, inaendesha tangu mapema mwezi Desemba mashambulizi ya anga nchini Syria.

"Tutaendelea na jihadi, tuvuke mipaka, na siku moja tutavamia nchi yako, ambapo tutawala kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu", mwanamgambo wa IS ameongeza.

"Kwa wale ambao wanataka kuendelea kupambana chini ya mwelekeo wa Cameron, (...): unawaza kweli kwamba serikali yako itakukumbuka wakati utakua umeanguka mikononi mwetu? Au watakutupilia kama walivyowatupilia wapelelezi hawa na wale waliokuja kabla yao? ", mwanamgambo wa Is amesema, akiwachagua watu watano kupiga magoti mbele yake.

Mwishoni mwa hotuba yake, watu hao watano wameuawa kwa kupigwa risasi kichwani.