FIFA-UFISADI

FIFA: Valcke, afutwa kazi katika mgogoro usiokuwa na mwisho

Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke katika mkutano na waandishi wa habari, Mei 30, 2015, Zurich.
Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke katika mkutano na waandishi wa habari, Mei 30, 2015, Zurich. AFP/AFP/

Mwezi mmoja na nusu kabla ya uchaguzi wa rais wa shirikisho la Soka Duniani (FIFA), vigogo wa shirikisho hilo wanaendelea kukabiliwa na hatua kali.

Matangazo ya kibiashara

Namba 2 wa FIFA Jérôme Valcke amefutwa kazi Jumatano hii baada ya kuhusishwa na mauzo ya tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2014, sehemu nyingine ya mgogoro mkubwa unaoikabili taasisi kuu ya mpira wa miguu.

Ni kwa uamuzi wa kamati ya dharura ambapo mkataba wa ajira kati ya FIFA na Jérôme Valcke, mwenye umri wa miaka 55, na mtu wa karibu wa Joseph Blatter tangu mwaka 2007, umevunjwa.

"Jérôme Valcke anaridhishwa na kila kitu kililiyokamilika chini ya utawala wake wa Katibu mkuu, ambapo Kombe mbili za dunia zikiwa ni miongoni mwa mafanikio katika historia ya soka, nchini Afrika Kusini na Brazil. Valcke ana imani kuwa, historia itakumbuka mchango wake kwa mchezo anaoupenda", amesema mwanasheria wake, raia wa Marekani, Barry Berke katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la Ufaransa AFP.

Chini ya mwezi mmoja, shirikisho la Soka Duniani limewapoteza viongozi wake vigogo watatu, kwani tangu Desemba 21, Sepp Blatter, rais wa FIFA aliyejiuzulu, na Michel Platini, rais wa shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), walisimamishwa kwa muda wa miaka 8 katika shughuli ya aina yoyote inayohusiana na mpira wa miguu.

Blatter, mwenye umri wa miaka 79, na Platini, mwenye umri wa miaka 60, waliadhibiwa na Mahakama ya ndani ya FIFA kwa kosa la malipo yenye utata ya Euro milioni 1,8 mwaka 2011 bila kuwa na mkataba wowote. Majaji wa FIFA waliona hayo kama "matumizi mabaya ya madaraka" na "mgogoro wa maslahi".

Hivi karibuni Michel Platini alijiondoa katika kinyan'ganyirio cha kuwania urais wa FIFA, uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 26 mjini Zurich, akibaini kwamba hana muda wa kutafuta wapiga kura.

Mpaka sasa watu watano ndio wanajulikana kama wagombea kwenye wadhifa huo: mjumbe wa zamani wa FIFA, Jérôme Champagne, Katibu mkuu wa shirikisho la Soka Ulaya Gianni Infantino, mfanyabiasahra wa Afrika Kusini Tokyo Sexwale, mwanamfalme wa Jordan Ali na rais wa Shirikisho la Soka barani Asia Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa.